Mwandishi Wetu
SIKU 10 kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Sita
wa Bunge, wabunge kutoka mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara wameunda umoja wa kuibana
Serikali bungeni wakitaka kupewa majibu ya kueleweka kuhusu suluhisho la
migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka
kwa watu wa karibu wa wabunge hao, huku baadhi yao wakithibitisha na kutotaka
majina yao kuandikwa gazetini, zinaeleza kuwa uamuzi huo unatokana na migogoro
ya makundi hayo kutopatiwa ufumbulizi, licha ya kuwepo muda mrefu na
kusababisha wananchi kupoteza maisha.
“Sisi wabunge lazima tusimame katika
nafasi yetu ya kutetea wananchi bila kujali itikadi za vyama vyetu,” alisema
mbunge mmoja kutoka mkoa wa Pwani.
Habari hizo zinaeleza kuwa wazo hilo
lililowaunganisha wabunge wa CCM, Chadema na CUF liliibuliwa na wabunge wa mkoa
wa Pwani na kuungwa mkono na wenzao wa
mikoa ya Mtwara na Lindi.
Februari mwaka jana katika mkutano wa
Bunge mjini Dodoma, wabunge wanaotoka kwenye mikoa ambayo Reli ya Kati inapita,
waliunda umoja kama huo, lakini wao walikuwa wakishinikiza ujenzi wa reli hiyo,
wakisema bila Serikali kusikiliza kilio chao, watahamasisha wenzao waisusie
bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Kufuatia sakata hilo, Serikali ilitoa
majibu kuhusu ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kutaja kiasi cha Sh trilioni 1
kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge).
“Ushawishi umekuwa mkubwa na tumeungwa mkono
na wabunge wengine wa mkoa wa Morogoro. Bado tunaendelea kushawishi wengine ili
wawe pamoja na sisi. Migogoro hii inawaumiza wananchi, lakini Serikali imekaa
kimya bila kuja na mkakati wa kueleweka,” alisema mmoja wa wabunge kutoka mkoa
wa Mtwara.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk
Charles Tizeba alipoulizwa kuhusu mkakati wa wabunge hao alisema, “Kwa sasa
Serikali ipo kazini jambo hili la migogoro ya wakulima na wafugaji linafanyiwa
kazi. Kuhusu mkakati wa wabunge hao siujui kwa kweli ila nitakutana nao bungeni
na tutakuwa na majibu ya kutosha kuwaridhisha.”
Mmoja wa wabunge hao kutoka Chadema
alisema Serikali haina dira wala mwelekeo kwa maelezo kuwa wakulima na wafugaji
wamekuwa wakiuana lakini hakuna waziri anayesema lolote na kusisitiza, “watatueleza
ndani ya bunge kazi yao ni nini.”
Katika mapendekezo hayo, wabunge hao
ambao wamekuwa wakijadili jambo hilo mara kwa mara sambamba na kupanga
mikakati, wameshauriana kuishauri Serikali kuipeleka Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi chini ya Ofisi ya Rais kwa usimamizi zaidi.
“Tatizo la wakulima na wafugaji halina
mwenyewe. Leo linaweza kutokea jimbo hili na kesho likatokea jimbo jingine. Si
suala la huyo wa Chadema au huyu wa CCM. Lazima tuungane kuhakikisha suluhisho
linapatikana,” alisema mbunge wa CCM mkoa wa Lindi.
0 comments:
Post a Comment