Peter Akaro
George Simbachawane |
SERIKALI
imefuta mwongozo uliotaka wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji kusitisha
matumizi ya mihuri, badala yake jambo hilo sasa litajadiliwa kwa kushirikiana ili
kufikia uamuzi utakaosaidia wananchi.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali
za Mitaa, George Simbachawane, alisema wenyeviti wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu ya kuhudumia wananchi, hivyo haoni sababu ya kulumbana muda huu.
“Ninasitisha
mwongozo uliotolewa hadi tukakaposhirikishana kwa kuangalia namna bora ya
kuhudumia wananchi.
“Hakukuwa
na ajenda yoyote ila ni kuweka utaratibu mzuri ambao tulilenga kudhibiti wanaotumia
mihuri kinyume na taratibu,” alisema.
Alisema
mwongozo huo haukuwa na dhamira ya kuwapunguzia wenyeviti mamlaka na heshima
zao, bali kuweka utendaji mzuri katika ngazi za chini za serikali.
“Mwongozo
ulitolewa kwa sababu ya matumizi mabaya ya mihuri inayofanywa na baadhi ya
wenyeviti, vijijini na hata mijini ambayo imechangia migogoro mingi ya ardhi
nchini,” alisema.
Alitolea
mfano sheria namba nne na namba tano za mwaka 1999 zinazoeleza mwisho wa Mwenyekiti
wa Kijiji kutoa ardhi kwa mwekezaji au mgeni kuwa ni ekari 50 lakini wapo ambao
wanatoa ardhi hadi ekari 100 na 1,000.
“Mahali
ambapo Mwenyekiti amesaini, akagonga na muhuri hati ile inahesabika ina nguvu
kisheria kama ilivyo hati inayotolewa na Wizara ya Ardhi, ingawa utoaji huo unakiuka
sheria,” alisema.
Alisema
mijini utawala wa ardhi unasimamiwa na sheria namba nane ya mwaka 2007 ambayo
inasema eneo likishakuwa la mipango miji, sheria ya vijiji inaondoka, lakini
hilo limekuwa likipuuzwa na ndiyo maana kumekuwa na migongano ya hati kwa
kutumia mihuri
Alisema
ipo sheria ambayo inasimamia vitendea kazi kwa wenyeviti wa serikali za mitaa
na vijiji ambayo ni Tangazo la Serikali namba tatu la mwaka 1994.
Sheria
hiyo inataja vitendea kazi vya Mwenyekiti kuwa ni Bendera yenye nembo ya halmashauri,
usajili wa wakazi wote, daftari la muhutasari ya vikao vya mtaa, ila haitaji
muhuri.
“Nguvu
ya Mwenyekiti haiko kwenye muhuri na ndiyo maana hata Rais hana muhuri isipokuwa
Katibu Mkuu Kiongozi, hivyo wenyeviti waelewe nguvu yao iko kwenye utendaji na
uamuzi,” alisema.
Uamuzi
huu wa Serikali umekuja siku moja baada ya wenyeviti wa serikali za mitaa
jijini Dar es Salaam kutangaza azma ya kugomea shughuli zao za usimamizi wa
amani na usalama kwenye maeneo yao na kuhudumia wananchi kutokana na mwongozo
wa kunyang’anywa mihuri.
0 comments:
Post a Comment