Edith Msuya
MTAALAMU wa elimu na mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, amemwomba Rais John
Magufuli aruhusu ajira za walimu wa vyuo vikuu nchini na hasa wenye kiwango cha
Shahada ya Uzamivu (PhD) ili kunusuru elimu ya vyuo vikuu.
Amesema hali iliyopo sasa ni changamoto
kubwa ya uhaba wa walimu hao kwenye vyuo vikuu nchini ikiwamo UDSM na kwa hali
hiyo wanafunzi wa vyuo vikuu wengi wao wanafundishwa na walimu wasiokuwa na PhD.
Profesa Mkumbo alitoa kauli hiyo Dar es
Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa HakiElimu wa mwaka 2017
hadi 2021 ambapo wadau wa elimu walipata fursa kujadili mafanikio na changamoto
ambazo zinakwamisha ukuaji elimu nchini.
Akiwasilisha mada, Profesa Mkumbo
alisema zipo changamoto nyingi na kwenye elimu ya juu, kuna uhaba mkubwa wa walimu
wenye PhD ambao ndio walipaswa kuwapo kufundisha wanafunzi hivyo kukosekana wa
kutosha kumesababisha walimu kuwa na wahadhiri wasaidizi wengi.
Alisema kwa mazingira hayo wahadhiri
waandamizi ni wachache na matokeo yake wasaidizi inabidi wawe wanaendelezwa
kitaaluma hadi kufikia sifa ya PhD na hicho ndicho kinafanyika sasa.
Alitolea mfano kuwa hata UDSM wahadhari
waandamizi wenye PhD ni wachache huku akieleza kuwa pamoja na uchache huo, Rais
Magufuli amekuwa akiteua wasomi hao serikalini na hivyo kuongeza uhaba wa
walimu wenye sifa kwenye chuo hicho.
Alisema ili kukabiliana na uhaba wa
wahadhiri wenye PhD UDSM ni vema Rais akaruhusu ajira za walimu wenye kiwango
hicho ili kuendelea kuzalisha na kupima wasomi ambao watakuwa msaada kwa Taifa.
Alifafanua kuwa UDSM kuna asilimia 41 ya
wahadhiri wenye PhD huku vyuo vingine hali ikiwa ni mbaya.
Alisema mbali ya uhaba huo kwenye vyuo
vikuu, pia kuna changamoto ya mfumo mzima wa elimu nchini kuanzia msingi,
sekondari hadi elimu ya juu.
Profesa Mkumbo alisema elimu ya msingi
haandai mwanafunzi kuwa na maarifa na kibaya zaidi hata wanaotoa elimu hiyo
wengi wao wamejikita kuangalia mwanafunzi anafaulu kwa alama gani, badala ya mwanafunzi
kupata maarifa ya aina gani ya kumsaidia kwenye maisha yake na Taifa kwa jumla.
0 comments:
Post a Comment