Suleiman Msuya
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa
kutumia takwimu rasmi na kuzingatia kanuni katika kuandika taarifa za aina hiyo,
ili kusaidia jamii.
Hayo yamesemwa na Mtakwimu Mkuu wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS), Emillian Karugendo, wakati akiwasilisha mada kwenye
semina elekezi kwa waandishi hao kuhusu Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na
Sheria ya Makosa ya Mitandao iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la
Internews, Dar es Salaam.
Alisema kuzi kuwa iwapo waandishi
watazingatia takwimu na kanuni katika mchakato wa
taarifa wanazotoa watasaidia jamii kupata elimu sahihi ya jambo husika.
Karugendo alisema msingi wa takwimu
rasmi utaonesha mfumo mzima wa uzalishaji, uchakataji na usambazaji taarifa
husika.
"Sisi NBS tunasimamia sheria na
kanuni kuhakikisha misingi ya kuandaa takwimu inafuatwa na si kukandamiza mtu,
hivyo taasisi na watu binafsi wanapaswa kutoa ushirikiano," alisema.
Mtakwimu huyo alisema baada ya sheria
hiyo kupitishwa, wamepokea maombi kutoka kwa watafiti ambao wanataka kukusanya
takwimu.
Alisema sheria yoyote haiwezi kuwa rafiki
kwa watu wote, hivyo kinachohitajika ni wadau kutoa mapendekezo katika
kuhakikisha kila mdau anakuwa salama.
Karugendo alisema kwa sasa wanajikita kwenye
utoaji elimu kwa wadau na jamii kwa ujumla jambo ambalo linaweza kutoa matokeo
chanya ya sheria hiyo.
Mwanasheria wa NBS, Oscar Mangula
alisema sheria hiyo imekuja kuiwezesha ofisi hiyo kuratibu mambo ya takwimu kwa
uwazi zaidi.
Alisema kwa sasa wamo kwenye mchakato wa
kukamilisha kanuni ili ziweze kufanya kazi pamoja na sheria.
Oscar alisema sheria hiyo inafanya kazi
Tanzania Bara na Zanzibar hasa upande wa sensa ya watu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Takwimu,
Dk Camilius Kasala alisema ili waandishi wa habari na watafiti waweze kushiriki
kwa amani katika utekelezaji wa sheria ni muhimu kusoma Takwimu.
Alisema iwapo waandishi watafanikiwa
kupata mafunzo ya takwimu, ni wazi kazi zitakwenda kwa uwiano sahihi.
"Pamoja na misingi mnayosimamia, mnapaswa
kuepuka msukumo, upendeleo na msimamo katika kazi ambazo ni taarifa za
takwimu," alisema.
Mwanasheria James Marenga alitoa mwito
kwa waandishi kusoma sheria hiyo kwa makini kwa kuwa hawako salama.
Alisema sheria hiyo inagusa watu wengi
hata ambao hawahusiki na takwimu.
0 comments:
Post a Comment