*Ni kuhusu kutohudhuria Mapinduzi Zanzibar
*Uamuzi wake wa kununua ndege 6 za ATCL
Mwandishi Wetu
Dk. John Magufuli |
NI kama amebadili gia angani. Rais John
Magufuli jana aliufanya mkoa wa Shinyanga kuwa wa kwanza kufanya sherehe za
Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya Tanzania Bara huku akieleza sababu za kufanya
hivyo, akizima minong’ono na hoja zilizozuka zikihoji sababu za yeye
kutohudhuria sherehe hizo visiwani.
Aidha, Dk Magufuli alitumia sherehe hizo
za miaka 53 ya Mapinduzi, kumjibu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu
lawama dhidi ya kununua ndege badala ya kuondolea wananchi shida ya maji.
Akihutubia wananchi kwenye uwanja wa
Kambarage Shinyanga Mjini, Rais Magufuli alisema aliamua kufanya sherehe za
Mapinduzi Shinyanga na kwamba kuanzia sasa sherehe zote za kitaifa zitakuwa
zikisherehekewa katika kila mkoa nchini.
Rais Magufuli alisema wakati yeye
akifanya sherehe hizo mkoani humo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk
Ali Mohammed Shein amempa Waziri wa Tamisemi Zanzibar, Haji Omari Kheir ili
kusherehekea sikukuu hiyo kama ilivyofanyika Zanzibar.
“Tunataka Mapinduzi yanufaishe wananchi
wote wa Tanzania kwa vitendo. Kwani kuna ubaya gani Mapinduzi yakisherehekewa
Zanzibar na Tanzania Bara, hakuna ubaya mtu akiwa na ‘bethidei’ ikasherehekewa
Zanzibar, ikasherehekewa pia Dodoma, zote ni sherehe.
“Watu wamezoea kila sherehe tujirunde
sehemu moja wakati tunaweza kutawanyika kila kona ya nchi hii na bado
tukasherehekea sikukuu yetu bila kuondoa maana iliyokuwapo mwanzo,” alisema
Rais Magufuli.
Alisema Mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar
miaka 53 iliyopita, ndiyo yamesababisha kuwepo kwa Tanzania ya sasa, huku
yakiwezesha pia Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa anayetoka Pemba kuwa Waziri.
Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo
kumtupia kijembe, Lowassa ambaye aligombea urais kupitia Chadema na kushindwa kwenye
Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka juzi.
Katika mikutano yake ya ndani, Lowassa
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alinukuliwa na vyombo vya habari akiponda
hatua ya Rais kununua ndege mbili aina ya Bombadier, akisema alipaswa kutengeneza
miundombinu ya maji kwanza badala ya kununua ndege.
Lakini jana akijibu hoja hiyo, bila
kutaja jina la Lowassa, Rais Magufuli alisema: “Wapo watu wamekuwa wakiponda
kila jambo ambalo Serikali inafanya, fikirieni tulikuwa hatuna ndege hata moja
ya Serikali, lakini leo tuna mbili lakini kuna watu wanasema tungeleta maji,
wakati yeye alikuwa Waziri husika na bado shida ya maji imeendelea kuwapo.”
Akizungumzia elimu, Rais Magufuli
alisema uamuzi wa Serikali kutoa elimu bure umechangia kuongeza idadi kubwa ya
watoto wanaosoma ambapo kwa mwaka uliokwisha, watoto waliojiunga na elimu ya
msingi walikuwa milioni mbili tofauti ya milioni moja mwaka juzi.
Rais pia alizungumzia elimu ya juu ambapo
alisema Serikali imefanikiwa kutoa mikopo kwa wanafunzi kulinganisha na miaka
ya nyuma ambapo mwaka jana kiasi cha Sh bilioni 500 zilitengwa kwa wanafunzi
120,000 sawa na asilimia 100 kulinganisha na Sh bilioni 373 zilizotengwa kwa
mwaka juzi kwa wanafunzi 85,000.
Kuhusu vita dhidi ya mafisadi, Rais
Magufuli alitaka Watanzania kuendelea kumwombea kwani kazi hiyo bila mkono wa
Mungu ni ngumu, huku akisisitiza kuwa anataka kuona masikini wakiishi kama malaika
huku waliozoea ‘kupiga dili’ wakiishi kama mashetani.
“Najitoa sadaka kwa ajili yenu na hii ni
kwa sababu watu walikuwa ‘wakipiga dili’ na kunufaisha matumbo yao kwa fedha za
maendeleo hivyo niwahakikishie kuwa Serikali ya Magufuli itapambana na
kuhakikisha hakuna watu wanatumia fedha za Watanzania kujinufaisha,” alisema.
Alitaka Watanzania kufanya kazi na
kuacha kulalamika kuwa fedha mifukoni zimekwisha na kusema wanaolalamika ni
waliokuwa wakitegemea fedha za ‘dili’ huku akiwauliza kuwa “kwani hapo mwanzo
zilikuwa zikigawiwa bure?”.
Wadau
Mapema wadau mbalimbali walitofautiana
kuhusu hatua Rais Magufuli kutohudhuria sherehe hizo.
Baadhi walisema hakuna tatizo kwa yeye
kutohudhuria sherehe hizo, huku wengine wakisema kwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania aliwajibika kwenda.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma
(Chauma), Hashim Rungwe alisema haikuwa na umuhimu wa yeye kuwapo kwani si
mgeni rasmi wa sherehe hizo na kubainisha kuwa hatua hiyo isingeathiri
chochote.
“Yeye hana mizinga pale wala chochote,
sioni mahala popote ambapo amekosea sana, hata asipokwenda haina madhara, si
mgeni rasmi kwamba asipokuwepo sherehe haifanyiki, yeye akienda ni kama mimi
tu,” alisema Rungwe.
Aidha, alisema kukosekana kwake labda ni
kujivunija heshima kwa hadhi yake kama Rais wa Jamuhuri ya Muungano ambapo
alisema masuala yote yanayohusu Muungano angetakiwa kushiriki.
Rungwe aliongeza kuwa Rais Magufuli
huhitajika Zanzibar inapokuwa katika tishio kama la kuvamia au kupoteza Dola
kwa kuwa yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu hivyo kuwajibika kutuma majeshi.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju
alisema tafsiri yake ni umuhimu wa sherehe zenyewe, akibainisha kuwa sherehe za
Mapinduzi ya Zanzibar ni mapindunzi ambayo kimsingi yalilenga kujitawala.
“Sasa hili tukio ni kubwa sana la
kihistoria, kitendo cha Rais kushindwa kupima umuhimu wa hivi vitu na kuheshimu
kumbukumbu kujua tulitoka wapi ni kitendo ambacho kinaonesha kuwapo changamoto
kwenye uongozi,” alisema Juju.
Alieleza kuwa kutokana na umuhimu wa
tukio hilo, alitakiwa kuwa mfano wa kuheshimu Mapinduzi hayo kwa kutambua
“tulikotoka na tunakoelekea”.
Katibu Mkuu wa National League for
Democracy (NLD), Tozi Matwanga alisema hajui Rais ataliambia nini Taifa kwa
kutohudhuria kwani ni sawa na kuonea Wazanzibari.
“Kwa kitendo hicho ameonea Wazanzibari
na Watanzania kwa ujumla, kwa sababu yeye ndiye mhimili wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania,” alisema Matwanga.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alisema hajui sababu ya Rais kutokwenda kwenye maadhimisho hayo.
“Siwezi kujua labla huenda ana nyingi au
anaumwa, hivyo mwulizeni kwanza Msigwa (Gerson) aseme kwa nini hajaenda ndiyo
uniulize mimi,” alisema Lissu.
0 comments:
Post a Comment