Salha Mohamed
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
inatarajia kwenda shuleni kufanya uchunguzi ili kubaini wenye matatizo ya moyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya JKCI kubaini
watoto kati ya miaka 10 hadi 18 ndiyo waathirika wa milango ya moyo huku
ikifanya upasuaji wa kubadilisha milango ya moyo (valves) ambayo haipitishi
damu vema.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Bashiri Nyangasa wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu upasuaji uliohusisha uvunaji wa mishipa ya damu mguuni
na kupandikiza katika mishipa ya moyo.
Upasuaji huo wa siku tano ulifanyika kwa
wagonjwa sita ulishirikisha jopo la madaktari kutoka hospitali ya Apolo,
Bangalore, India.
“Tuna mpango wa kuzungumza na shule na
kaya kwa ajili ya kupata wagonjwa kwa ajili ya upasuaji, wagonjwa wengi ni kati
ya miaka 10 hadi 18 ndiyo waathirika wakubwa wa kuharibika kwa milango ya moyo,”
alisema.
Alisema: “Upasuaji huu ulifanyika bila
kutumia mashine ya mapafu na moyo. Tumemfanyia mgonjwa upasuaji wa milango
miwili ya moyo ambayo iliharibika sana”.
Alisema ubadilishaji wa milango hiyo
iliyoharibika ulifanyika kwa kutanuliwa kishina cha mshipa mkubwa wa moyo kwa
kutumia mfuko wa moyo.
Dk Nyangasa alisema kupitia upasuaji huo,
Serikali iliokoa Sh milioni 174 kama ingepeleka wagonjwa India.
Mkurugenzi wa Tiba ya Afya ya Moyo JKCI,
Dk Peter Kisenge alisema kwa kuanza mwaka wameanza na kambi ya Apolo ambapo
wiki ijayo watakuwa na kambi ya madaktari wa Marekani.
“Wao watafanya tiba ya moyo bila
upasuaji na kuweka kizibua njia kwa wagonjwa 15 kuanzia Januari 23 hadi 29.
Februari 4 watakuja wa Saudi Arabia ambao watafanya matibabu bila kupasua moyo
kwa wagonjwa 55,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya jopo la madaktari
wa Apolo, Dk Sathyaki Nambala alisema ni mara ya nne kufanya upasuaji
hospitalini hapo kulikokuwa na upungufu wa madaktari na vifaa.
“Tulipokuja mara ya mwisho kulikuwa na
upungufu wa vifaa na madaktari lakini sasa vyote vipo, kikubwa ni kushirikiana
na timu kufundishwa upasuaji na kupata elimu
zaidi,” alisema.
Alisema wanatarajia kuona madaktari hao
wakijitegemea katika kufanya upasuaji mgumu zaidi huku akiitaka Serikali kupeleka
madaktari nje ya nchi kujifunza ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje
ya nchi.
0 comments:
Post a Comment