Mtoto wa miaka 10 ajinyonga


Wankyo Gati, Arusha

MTOTO wa darasa la tano katika shule ya msingi ya Engosengiu, Caren Amon (10), amejinyonga kwa kamba.

Mtoto huyo alifanya kitendo hicho kwenye kibanda cha kufugia kuku nyumbani kwao mtaa wa Muriet kata ya Sokoni One mjini hapa.

Caren ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia yao ya watoto wawili wa kike kifo chake kiliibua hisia za watu wengi ambao walishindwa kuamini kilichotokea.

Mdogo wa marehemu, Catherine (6) aliyekuwa akicheza na dada yake nyumbani kwao alisema wakati wanacheza, dada yake aliokota kamba iliyoletwa na mtoto wa jirani na kumwambia mdogo wake kuwa anataka kujinyonga.

Alisema alifanya hivyo huku mdogo wake akijitahidi kuokoa maisha ya dada yake kwa kupanda kwenye benchi akakata kamba na akaanguka chini na yeye kuita majirani.

Mama wa marehemu, Beatrice Mamkwe alieleza kutoamini kilichompata mtoto wake, kwani waliagana vizuri asubuhi akienda kazini na alishituka kupigiwa simu kuwa nyumbani kuna matatizo.

Pia aliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kifo hicho ili kuondoa maswali ya sababu za mtoto huyo kujinyonga.

Baba wa marehemu, Amon Swai alisema mara ya mwisho alizungumza na mtoto wake akimtaka asome sana kwani darasa analoingia ni jipya na kuwa atakutana na walimu wapya na hivyo awe mtii shuleni, lakini suala la msiba haliamini na hataki kuamini hata sasa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni One, Petro Mollel alisema alipokea taarifa hiyo kwa mshituko na kwamba anaiomba familia iendelee kuvuta subira wakati uchunguzi wa  chanzo cha tukio hilo kikitafutwa hasa ikizingatiwa uamuzi huo mzito na umri wa mtoto huyo.

Majirani, Zena Ali na Mollel Joseph kwa nyakati tofauti walisema kwa hali hiyo wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao kwa kuwaacha wakiwa na watu wakubwa ili kuzuia hatari zinazoweza kuepukwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo