Serikali yaokoa moja, yakoleza machungu ya lingine
Celina Mathew
UGUMU wa kawaida wa Januari, mwaka huu umeongezeka baada
ya kuongezeka kwa mambo manne, juu ya gharama za kawaida za mwezi huo.
Kwa kawaida Januari huwa ngumu kutokana na sehemu kubwa
ya mapato ya Desemba kutumika katika sikukuu za mwisho wa mwaka, huku gharama
za ada za shule, vifaa vya shule na kodi za nyumba vikianza kudaiwa mwanzoni
mwa mwaka.
Mwaka huu Januari imeanza na mizigo ya ziada ya kupanda
kwa bei za chakula, kuongezeka kwa kasi na mbinu za kudai madeni ya benki,
msako wa nyumba kwa nyumba wa wadaiwa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HESLB), huku Serikali ikinusuru ongezeko la bei ya umeme.
Bei ya chakula, ukame
Wiki hii gazeti hili lilifanya uchunguzi wa bei za
vyakula katika mikoa ya Mara, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro, Simiyu, Shinyanga,
Singida, Tabora, Arusha, Manyara na Tanga na kukuta zimekuwa zikiongezeka kila
kukicha.
Taarifa zinaonesha kwamba wilayani Bunda, Mara, bei ya
chakula imepanda kutoka Sh 14,500 kwa debe la mahindi hadi Sh. 20,000; mtama
kutoka Sh 10,000 hadi Sh 17,500; unga wa muhogo kutoka Sh 12,500 hadi Sh 17,500
na ulezi unauzwa Sh 30,000 kwa debe.
Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka kwenye soko kuu la
mjini humo na mji mdogo wa Kibara jimboni Mwibara, walisema bei ya chakula
imepanda kutokana na upungufu mkubwa wa nafaka.
Mkazi wa eneo hilo, Esther Samson alisema hali hiyo
ilisababishwa na mvua kutonyesha wilayani humo kwa kipindi kirefu na
kusababisha mazao yaliyolimwa kunyauka.
Esther alisema wamekuwa wakiuza chakula wanachopata
kutoka mikoa jirani kwa bei ya juu ili kurudisha mtaji na kupata faida kidogo.
“Hali ya chakula kwenye soko letu ni mbaya maana
kimepanda kutokana na sisi tunavyouziwa kwa bei ya juu. Na hii hali tuseme
ilianza Agosti na Septemba mwaka jana. Sasa hivi gunia la mahindi tunanunua
kati ya Sh 110,000 na Sh 120,000,” alisema.
Katika mikoa ya Pwani na Morogoro, ambako pamoja na
wananchi kulia bei kubwa ya chakula hata mifugo imekuwa ikifa kutokana na
ukame.
Mfugaji Solengei Saitoti wa Morogoro alisema ameshapoteza
mifugo zaidi ya 50 huku kukiwa hakuna dalili za mvua kunyesha ili kuikoa.
Bodi ya Mikopo
Wakati bei ya chakula ikiongeza ugumu wa maisha, HESLB
imeanza mwaka huu na msako wa nyumba kwa nyumba wa wadaiwa sugu, ulioanzia
Shirika la Ndege la Precision Air.
Mbali na Precision, wasaka madeni wa bodi hiyo
wameshafika kwenye Kampuni ya Mantrac na kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi
(SBC Tanzania Limited), kufuatilia waajiri wasiotekeleza sheria ya bodi ya kupeleka
makato ya wanufaika wa mikopo waliowaajiri.
Jumatano ya mwisho ya mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa
HESLB, Abdul-Razaq Badru, alitoa siku 14 kwa kila mwajiri nchini kupitia upya
taarifa za waajiriwa na ambao hawatafanya hivyo na kutoa taarifa za wadaiwa wa
Bodi hiyo, watatakiwa kulipa faini isiyopungua makato hayo, au kifungo cha
miezi 36 jela.
Mbaya zaidi Badru alisema Bodi hiyo inakusudia kufanya
marekebisho ya sheria, ili wanufaika wa mikopo hiyo waanze kukatwa asilimia 15
ya mshahara kwaajili ya kulipa deni lao, badala ya makato ya sasa ya asilimia
nane ya mshahara.
Kuhusu waliojiajiri na ambao hawako katika mfumo rasmi, Badru
alisema nao wanapaswa kulipa Sh 100,000 au asilimia 10 ya kipato chao
kinachotozwa kodi kila mwezi.
Madeni ya Benki
Katika kuonesha mabenki yamedhamiria kumalizana na
wadaiwa wao, wiki hii gazeti hili limeshuhudia nyumba zaidi ya 38 katika mikoa
mbalimbali nchini, zikitangazwa kupigwa mnada na Benki ya NMB kutokana na
wahusika walioziweka dhamana kushindwa kulipa mikopo yao kwa wakati.
Nyumba hizo zinazotarajiwa kupigwa mnada Januari 21 mwaka
huu ziko Tunduma, Sumbawanga, Mbozi, Newala, Kibaya, Gairo, Itigi, Turiani,
Songea, Wami, Kyela, Usongwe, Kitunda Dar es Salaam, Hai Kilimanjaro na
Simanjiro Manyara.
Mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na taarifa mbalimbali za
benki kuingia mkataba na taasisi za udalali na kupiga mnada mali zilizowekwa
dhamana na wateja waliochukua mikopo na kushindwa kuirejesha.
Gazeti moja la kila siku nchini lilirekodi idadi kubwa ya
matangazo ya benki na taasisi za fedha, yakitishia kupiga mnada mali za wateja
wao kutokana na kushindwa kurejesha madeni, hali inayoonesha huenda ikatekelezwa
kwa uhalisia mwaka huu.
Miongoni mwa waathirika wa marejesho mwaka jana ilikuwa
Benki ya Twiga, ambayo ilifungwa kwa muda kutokana na kushindwa kurejeshewa
fedha ilizokopesha wateja, hali iliyotajwa kuathiri benki nyingi, ambazo
zilianza kufuatilia madeni yao na tayari zimeongeza kasi ya kudai mwaka huu.
Bei ya Umeme
Miongoni mwa magumu yaliyotajwa mwishoni kabisa mwa mwaka
jana, ni ongezeko la umeme la wastani wa asilimia nane, ambapo kila mwananchi
alikuwa alazimike kutumia zaidi kupata huduma hiyo.
Ongezeko hilo lisingechagua wa mijini wala wa vijijini
kwa kuwa wanaotumia nishati hiyo kwa sasa wameongezeka mpaka vijijini na kwa
viwandani, kulikuwa na uwezekano wa bei hiyo mpya ya umeme, kuchangia ongezeko
la bidhaa za viwandani zinazozalishwa kwa kutumia nishati hiyo.
Bei hiyo mpya ya umeme, ilitangazwa Ijumaa ya mwisho ya
mwaka jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, ambaye aliweka wazi kuwa ilikuwa ianze mapema
Januari hii.
Serikali yapunguza
Hata hivyo ndani ya muda mfupi, Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliitaka Ewura kusitisha bei mpya ya umeme
iliyotangazwa na Ngamlamgosi.
Akizungumza na gazeti hili kwa na vyombo mbalimbali vya
habari, Prof Muhongo alisema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu kadhaa,
ikiwamo kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.
“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei
kupanda, wao wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni
kwamba Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la
kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti
wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.
“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita
Ewura na Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao
wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.
Baada ya hatua hiyo, Rais Magufuli alimpongeza Profesa
Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme na kueleza kuwa
waliopandisha umeme hawakumuuliza yeye wala waziri mwenye dhamana ya nishati, Makamu
wa Rais, Waziri Mkuu badala yake walifanya maamuzi yake peke yao bila
kushirikisha mamlaka nyingine.
“Namshukuru waziri wa nishati kwamba ameshatengua maamuzi
hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda.” Rais Magufuli alisema haiwezekani watu
mnapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya
nchi ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu
maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo
chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei
ya umeme, Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana nalizungumza hili kwamba majipu
bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba sana Watanzania
muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni kwenda na wananchi wa
kipato cha chini.”
Yakoleza machungu
Wakati Serikali ikiwapunguzia mzigo Watanzania kwa kuzuia
kupanda kwa bei ya umeme, imekwepa kushughulikia ongezeko la bei ya chakula,
huku Rais Magufuli akisema taarifa zinazoenezwa kuhusu nchi kukumbwa na njaa si
za kweli na kuwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia chakula.
Akihutubia wananchi wa Bariadi wiki hii alikokwenda
kuwashukuru na kuzindua ujenzi wa barabara na hospitali ya mkoa wa Simiyu, Rais
alituhumu baadhi ya wafanyabiashara walioingiza mahindi nchini na kutafuta njia
ya kuyauza.
“Kuna wanasiasa na baadhi ya waandishi wa habari
wanaotumika na wafanyabiashara walioingiza mahindi kwa njia zao na sasa
wanatumia kisingizio cha njaa ili kuuza mahindi hayo,” alisema Rais.
Alisisitiza kulima mazao yanayostahimili ukame na wenye
uwezo wa kumwagilia wafanye hivyo ili kuondokana na njaa kama itatokea mvua
zisinyeshe.
“Inashangaza mtu kulima mahindi ambayo yanahitaji maji
mengi na kuacha kulima mtama ambao hauhitaji maji mengi, mtu analima mahindi
kandoni mwa ziwa, lakini anashindwa hata kuchukua ndoo kuchota maji na kumwagilia,”
alisema Rais.
Akisisitiza taarifa za madai ya njaa, rais alitolea mfano
wa ng’ombe 17,000 kufa kwa njaa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, akisema hiyo
ni taarifa ya kutunga.
“Haiwezekani unaona ng’ombe mmoja anakufa, wa pili, 100…
ng’ombe elfu…wanakufa unaangalia tu kwa nini usiwauze ukanunua chakula,
ukanunua mahindi? Hii haiingii akilini,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza
kutokuwapo njaa nchini.
Hata hivyo, alirudia kauli yake kwamba serikali haina
shamba hivyo watakaokumbwa na njaa kutokana na kutolima, wasitarajie Serikali
iwapelekee chakula na badala yake wafanye kazi ya kujizalishia chakula.
“Hata Baba Askofu yuko hapa, anajua kwamba maandiko
yanasema asiyefanya kazi na asile … usipofanya kazi ukakosa chakula basi ufe
tu,” alisema Rais na kuwataka Watanzania kujiandaa kusikia na kuukubali ukweli.
“Kama mlizoea kusikia mazuri tu na sasa mjiandae pia
kusikia mabaya, mimi nitasema ukweli daima, siwezi kuita jiwe mchanga
uliojikusanya,” alisema.
0 comments:
Post a Comment