Mwandishi Wetu, Dodoma
WABUNGE wametakiwa kuielewa dhana ya
ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji ili kuwa mstari wa mbele kuelimisha
wananchi kushiriki shughuli za kiuchumi na uwekezaji nchini.
Mwito huo umetolewa na Serikali kupitia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Jenista Mhagama aliyesema wabunge kama wawakilishi wa wananchi, wana
nafasi kubwa ya kuwaelimisha kuhusu kuwawezesha Watanzania kuwa sehemu kubwa ya
wamiliki wa uchumi.
“Mafunzo haya yanatolewa kwenu kusaidia
kuleta mabadiliko chanya na jamii zitashirikishwa kikamilifu katika uwekezaji
unaofanywa katika maeneo yao kupitia ninyi wabunge,” alisema Waziri Mhagama.
Akizungumza kwenye Semina Elekezi kwa
Kamati za Bunge juu ya ushiriki wa wananchi katika uwekezaji iliyoandaliwa na Baraza
la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) mwishoni mwa wiki mjini hapa,
Mhagama alisema wakati umefika kwa Watanzania kunufaika na uwekezaji.
“Ni muhimu wananchi katika sehemu ambapo
viwanda au miradi inaanzishwa kushirikishwa hatua za awali za uwekezaji au
utekelezaji wa miradi,” alisema Waziri na kuongezea kuwa lengo la kufanya hivyo ni
kuhakikisha kuna uwazi na wananchi wajione ni sehemu ya uamuzi.
Alisema mafunzo hayo kwa kamati za Bunge
pia yametoa nafasi kwa wabunge kutambua majukumu ya NEEC ambalo ndilo lenye
dhamana ya kuratibu shughuli zote za uwezeshaji nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dk John
Jingu alisema uhusiano wa karibu kati ya wawekezaji na wananchi wa eneo la
mradi unatakiwa kuimarishwa ili wananchi wanufaike na uwekezaji wa miradi kwenye
maeneo yao.
“Changamoto kubwa ni ujuzi wa wananchi katika
uwekezaji na ushiriki wao,” alisema Dk Jingu na kuongeza kuwa Baraza
limejipanga kuhakikisha wananchi wanapewa elimu ya namna bora ya kushiriki
uwekezaji na kukuza uchumi wao.
Mbunge wa Muheza ambaye ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema semina hiyo ilikuwa na
umuhimu mkubwa kwa wabunge, kwani itawasaidia kuwaelimisha wananchi juu ya
ushiriki wao kwenye miradi inayofanyika kwenye maeneo yao.
“Tuna kila sababu za kuelimisha wananchi
wetu juu ya kuongeza thamani ya bidhaa ili kuendana na matakwa ya wawekezaji,” alisema
Balozi Adadi na kutaka sheria zinalinde wazawa katika ushiriki wao kwenye
uwekezaji.
Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna
Tibaijuka alisema ni vema Baraza na wadau wengine watathmini mambo
yaliyofanyika na yanayotarajia kufanyika ili watu wote wazungumze lugha moja
juu ya ushiriki wa wananchi kwenye uwekezaji.
Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa
alisema lengo kuu la semina hiyo kwa wabunge ni kuwafahamisha majukumu ya Baraza
na mchango wao katika dhana ya ushiriki wa wananchi kwenye uwekezaji.
Jumla ya wajumbe 152 wa kamati za Bunge
walihudhuria semina hiyo iliyodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP).
0 comments:
Post a Comment