*Azuia wahamiaji kutoka mataifa ya Kiislamu
*Asisitiza kuanzaujenzi wa ukuta wa
Mexico
WASHINGTON, DC, Marekani
Donald Trump |
RAIS Donald Trump ameanza kuchukua hatua
za kiutendaji kuhusu uhamiaji, akianza na kuimarisha ulinzi mpakani – ikiwa ni
pamoja na kutekeleza mapendekezo yake ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa
Marekani na Mexico.
Rais pia atachukua hatua katika siku
chache zijazo za kupiga marufuku kwa muda uhamiaji wa watu kutoka nchi za
Kiislamu zenye viashiria vya ‘tishio la usalama kwa taifa’ – ambazo ni Syria,
Iran, Iraki, Libya, Yemen, Sudan na Somalia.
Halikadhalika, Trump amejipanga kusaini
hatua zingine za ndani kuhusu kuimarisha masuala ya uhamiaji ikiwa ni pamoja na
kulenga majiji ambayo ni kimbilio la wengi, lakini yanashindwa kuwashitaki
wahamiaji wasio na nyaraka muhimu.
Hata hivyo, taarifa zilisema pamoja na
jana kuidhinisha kuanza kwa ujenzi wa ukuta huo, masuala mengine ya uhamiaji
ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku watu kutoka nchi za Kiislamu kuingia
Marekani, yataanza kutekelezwa baadaye wiki hii.
Juzi Rais alituma ujumbe kupitia mtandao
wa kijamii wa Twitter akielezea juu ya matamko mazito aliyopanga kuyatoa jana:
“Kesho ni siku kubwa kwa usalama wa Taifa …miongoni mwa mambo mengine,
tutajenga ukuta huo!”
Maelekezo hayo mapya ya Trump pia
yatazuia wakimbizi wengi kuingia nchini wakiwamo wa kutoka Syria wakati
michakato ya mchujo ikifanyika.
Tofauti pekee ni waumini wachache
wanaokimbia ghasia – ambayo itahusu Wakristo wanaokimbia Syria na nchi zingine
zenye Waislamu wengi, kwa mujibu wa wasaidizi wengi wa Bunge na wataalamu wa
uhamiaji walioelezwa kuhusu suala hilo.
Mipango iliyopendekezwa ni pamoja na
kusimamishwa kwa takriban miezi minne kwa ruhusa ya wakimbizi kuingia nchini,
lakini pia marufuku ya muda mfupi ya wahamiaji kuingia nchini kutoka nchi zenye
Waislamu wengi, kwa mujibu wa wawakilishi wa shirika la sera ya umma ambalo
linafuatilia masuala ya wakimbizi.
Pia kutakuwa na utofauti katika kuzuia
wakimbizi ambao wanakimbia unyanyasaji wa kidini, hasa kama dini yao ina watu
wachache ndani ya nchi husika. Hiyo itahusu Wakristo wanaokimbia nchi zenye
Waislamu wengi.
Rais huyu anayetoka chama cha Republican
alitarajiwa jana kusaini amri hizo jijini hapa kwenye Wizara ya Usalama wa
Ndani, ambayo majukumu yake ni pamoja na uhamiaji na usalama wa mipaka.
Akiwa kwenye kampeni, Trump alipendekeza
kuwekwa marufuku ya muda dhidi ya Waislamu wanaoingia nchini, lengo likiwa ni
kulinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kijihadi.
Trump na Mwanasheria Mkuu mteule, Seneta
Jeff Sessions walishasema watajielekeza katika kubana nchi ambazo wahamiaji wao
wanaweza kuwa tishio, kuliko kupiga marufuku watu wa dini fulani.
Wafuasi wengi wa Trump walishutumu
uamuzi wa Rais wa Democratic, Barack Obama wa kuongeza idadi ya wakimbizi wa
Syria waliosajiliwa nchini, kwa hofu kwamba waliokimbia vita vya wenyewe kwa
wenyewe nchini humo, wanaweza wakatekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini.
Wapinzani wa sera za Trump wanaweza
kufungua pingamizi la kisheria kama nchi zote zinatazoguswa na marufuku hiyo ni
zenye Waislamu wengi, alisema mtaalamu wa masuala ya uhamiaji, Hiroshi Motomura
wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Los Angeles. Hoja za kisheria zitaweza
kudai kwamba amri hizo zinabagua dini fulani, hatua ambayo ni kinyume cha
Katiba, alisema.
“Kauli zake wakati wa kampeni na baadhi
ya watu kwenye timu yake, zililenga zaidi dini kama lengo mahsusi,” Motomura
alisema.
Stephen Legomsky ambaye alikuwa mshauri
mkuu kwenye Huduma za Uraia na Uhamiaji nchini wakati wa utawala wa Obama,
alisema Rais ana mamlaka ya kudhibiti uingiaji wakimbizi nchini na utoaji viza
kwa nchi mahsusi kama utawala utaona kwamba ni kwa maslahi ya umma.
“Kwa mtazamo wa kisheria, hiyo itakuwa
ndani ya haki zake za kisheria,” alisema Legomsky profesa katika Shule ya
Sheria ya Chuo Kikuu cha Washington kilichoko St. Louis. “Lakini kwa mtazamo wa
kisera, litakuwa ni wazo la kushangaza, kwa sababu kuna haki ya mahitaji ya
kibinadamu kwa wakimbizi.”
Ili kuzuia watu kutoka nchi hizo kuingia
nchini, Trump anaweza kuagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuacha kutoa viza kwa watu
wa mataifa hayo, kwa mujibu wa vyanzo vinavyohusika na mchakato wa utoaji viza.
Anaweza pia akaagiza wanaohusika na
Ulinzi wa Forodha na Mipaka ya Marekani kuzuia wenye viza tayari wanaotoka nchi
hizo kuingia nchini.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Sean
Spicer alisema juzi, kwamba Wizara za Mambo ya Nje na Usalama wa Ndani, ndizo
zitashughulikia mchakato wa uchuchaji mara
tu mteule atakayeongoza Wizara ya Mambo ya Nje, Rex Tillerson atakaposimikwa
rasmi.
Hatua zingine zitajumuisha maelekezo kwa
mashirika yote kukamilisha kazi kwenye mfumo wa utambuzi wa wasio raia
wanaoingia au kuondoka nchini, na kuendesha msako dhidi ya wahamiaji wanaohudumiwa na serikali bila halali,
kwa mujibu wa wasaidizi wa Bunge na wataalamu wa uhamiaji.
Akiwa rais, Trump anaweza pia akaagiza
kusimamishwa kwa michakato yote ya kupokea wakimbizi. Rais George W. Bush
alitumia madaraka hayo mara baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11.
Msisitizo wa Trump kwamba Mexico ndiyo
itakayogharimia ujenzi wa ukuta ni miongoni mwa mapendekezo maarufu
yaliyotawala kampeni zake ambayo kila mara yalipokewa kwa shangwe kwenye
mikutano yake. Hata hivyo, Mexico mara kwa mara imesisitiza kuwa haitagharimia
chochote.
Maoni
Akizungumzia uamuzi huo wa Trump, Shekhe
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema anachokifanya Trump ni
mwendelezo wa kujenga uadui na chuki kwa
Waislamu huku akisisitiza kuwa kitendo hicho kitafanya waumini wa dini
duniani wamchukie yeye na Marekani.
“Huu ni mwendelezo wa chuki kwa
Waislamu, matendo ya kigaidi hayafanywi na Waislamu jina la mtu haliwakilishi
tabia yake, akumbuke kuwa Waislamu hawapo kwenye mataifa hayo bali wako dunia
nzima,” alisema.
Alisema suala hilo litamletea shida
kwenye utawala wake hasa kiuhusiano na mataifa mengine na hata raia wake
watachukiwa na Ulimwengu.
Aliyekuwa Mjumbe wa Bunge la Mabadiliko
ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema Trump amefanya uamuzi huo bila
kuangalia matokeo ya baadaye kwa Taifa hilo huku akiongeza kuwa suala hilo
linaweza kuleta vurugu na hali mbaya kiuchumi.
Alisisitiza kuwa kuna raia wanaotoka
mataifa hayo wanaojishughulisha na biashara, hivyo hutumia usafiri wa anga na
maji kuingia nchi hiyo, hivyo agizo hilo litasababisha biashara kuwa ngumu.
“Trump ameamua kabla ya kujua matokeo
yake yatakuwa nini, ni jambo litakaloleta vurugu kwenye usafiri wa anga na
maji, si wote wanaoingia Marekani ni wakimbizi bali wanaishi kwa shughuli za
kibiashara,” alisema Mwesiga.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema anachofanya Trump si sahihi,
kwani mtu hawezi kuzuiwa kuingia nchi nyingine kwa kuangalia dini yake huku akiongeza kuwa kufanya hivyo
ni kinyume na Sheria za Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.
Alisema Marekani ikianza kutekeleza
sheria hiyo, itakwenda kinyume na matakwa ya Shirika la Haki za Binadamu
Duniani, ingawa Taifa hilo lina utaratibu na sheria zake.
Mjumbe wa Wainjilisti wa Kikristo
Tanzania (UWAKITA), Elieza Shinza alisema jambo aliloamua kiongozi huyo ni
sahihi, kwa kuwa mataifa hayo yana ajenda ya kueneza Uislamu duniani kwa njia
yoyote ile, hivyo hata hilo lisipojitokeza leo linaweza kujitokeza miaka 20
ijayo.
“Mtazamo wetu tunajiuliza kwa watu hawa
wakimbilie Marekani wasiende mataifa mengine ndipo tukagundua kuwapo mpango
mkakati wa kueneza Uislamu,” alisisitiza.
Pia alisema inavyoonekana jinsi
wanavyozidi kuongezeka wanaweza kuanza kufunga ndoa na kuzaliana, hali
inayotishia huenda baadaye wakaja kuwa viongozi ndani ya Taifa hilo.
*Imeandikwa na Hussein Ndubikile na mitandao
0 comments:
Post a Comment