Dalila Sharif
WENYEVITI 400 na wajumbe 130 wa serikali
za mitaa mkoa wa Dar es Salaam wamejivua madaraka kwa kutoshiriki kutoa huduma
kwenye mitaa yao, ikiwa ni baada ya Serikali kuwaagiza kurejesha mihuri yake
waliyokuwa wakiitumia katika kazi zao.
Mbali na kutangaza kujivua madaraka,
wenyeviti hao wamedai kuwa watalifikisha shauri hilo mahakamani ili kupata
tafsiri ya kisheria juu ya utendaji kazi wao.
Tamko hilo lilitolewa jana Dar es Salaam
na katibu wa wenyeviti hao, Mariam Machicha kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi
wa TCC Chang’ombe.
Mariam alisema kwa mujibu wa tamko la Serikali
Novemba 30 mwaka jana barua kutoka Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa ikisainiwa na Katibu Mkuu Musa Iyombe, kuhusu mwongozo wa matumizi ya
mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji:
“Mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji, atatakiwa awe na bendera
yenye nembo ya Halmashauri, rejesta ya wakazi wote wa mtaa na daftari la mihutasari
ya vikao vya mtaa,” alisema Mariam.
Aliongeza kuwa kutokana na tamko hilo
wenyeviti wa mkoa wa Dar es Salaam, walikubaliana kurudisha mihuri ya Halmashauri
kwenye manispaa walizochukulia na kutoa tamko lao kwamba:
“Wenyeviti wote hawatashiriki vikao vya
kamati za maendeleo ya kata na hawatafika ofisi za serikali za mitaa kutoa
huduma za kijamii kwa wananchi wa maeneo yao.
“Kutokana na hili wenyeviti tunakubali
kwamba kitendo hiki cha kutotumia mihuri kitasababisha athari kubwa katika mfumo
wa uongozi na utoaji huduma kwa umma.”
Mariam alisema wenyeviti hao watashindwa
kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati wote na kuanzia sasa hawatasimamia ulinzi
na usalama wa wananchi kwenye mitaa yao.
“Kwa hali hiyo, hususan kwa watumizi ya
vyombo vya moto kama silaha, hatutasaini na wananchi watatangatanga na kupata
usumbufu wa kupata huduma kwenye ofisi za kata kwa sababu watendaji wengi hawajui
matatizo ya wananchi,” alisema Mariam.
Kiongozi wa wenyeviti wa mkoa wa Dar es
Salaam, Juma Mgendwa aliwataka wenyeviti hao kurudisha mihuri kwenye manispaa
zao na walioichonga wenyewe waache kuitumia.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva aliwataka
wenyeviti hao kutii agizo la Serikali na kuendelea na majukumu yao kwa kushirikiana
na watendaji wa mitaa kutoa huduma kwa
jamii.
“Ni vema kuwa na busara na kutekeleza
tamko hilo, kwa kuwa wapo baadhi walioanza kurudisha mihuri hiyo, hivyo ni vema
hatua hii ikafanyika kwa amani,” alisema
Lyaniva.
0 comments:
Post a Comment