John Banda, DODOMA
WANANCHI wa kata ya Msalato katika
Manispaa ya Dodoma jana wamegomea taarifa ya mapato na matumizi iliyosomwa na
Ofisa Mtendaji, Herman Malindila na kusababisha vurugu kubwa kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika eneo la Mnadani.
Katika mkutano huo uliofurika umati wa
wakazi wa eneo hilo, wananchi walimtaka mwakilishi wa mkuu wa wilaya, Vicent
Leo kuondoka na Ofisa Mtendaji huyo ili na wao washughulike na Diwani wa Kata,
Alli Mohamed na wenyeviti watatu wa
mitaa.
Chanzo cha vurugu hizo zilitokana na
wananchi kuzipinga taarifa ya diwani na Ofisa Mtendaji wake ambao kwa nyakati
tofauti walisoma taarifa ambazo zilijaa udanganyifu, huku Mwenyekiti wa Mtaa wa
Msalato Emanuel Mazengo wakipingwa hadharani kuhusu kutolewa kwa ardhi kwa
mwekezaji.
Kata ya Msalato ambayo ni maarufu kwa
kuwepo mnada ina vyanzo vingi vya mapato, lakini kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wananchi
wamedai kuwa hawajasomewa taarifa ya mapato na matumizi.
Diwani Mohamed alikanusha madai ya kuuza
ardhi wala kuitoa kwa mwekezaji licha ya mwekezaji huyo ambaye alijitambulisha
kuwa ni mkazi wa eneo hilo kutamka hadharani kuwa alichukua ardhi hiyo kwa
kupewa na viongozi akiwemo diwani.
“Ndugu zangu ninawahakikisheni kuwa mimi
sihusiki na wala sijashirikishwa na jambo lolote, kesho nitakuwa ofisini hivyo
naomba Mwenyekiti na mwekezaji aliyemtaja kwa jina la Paloline Erenest waje ofisini tuzungumze vingine nitawapeleka
polisi kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mnaninzingizia ” alisema Mohamed.
Naye Mwenyekiti wa mtaa huo wa msalato A
Emanuel Mazengo alikanusha kuuza ardhi hiyo lakini akasema alikuwa akijua
kilichokuwa kinaendelea chini ya mwekezaji huyo ambaye alikuwa amesaidia pia
pamoja na kuchonga barabara ndani ya mtaa wake.
Kwa upande wake Mtendaji Malindila
alisoma mapato ya machinjio tu lakini alipoulizwa maswali mengi alikosa majibu
hivyo akashindwa kusoma mapato mengine ikiwemo pango la minara ya simu, gulio
na vyanzo vingine.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya aliamuru
mkutano huo kufungwa baada ya kelele nyingi ambazo zilisababishwa na mapungufu
katika usomaji wa taarifa hasa ya mapato na matumizi iliyowasilishwa na
Mtedaji.
Leo aliwataka wananchi kutokuchukua
sheria mkononi ikiwemo ya kufunga ofisi kama walivyotaka kwani litakuwa ni kosa
na badala yake wasubiri majibu kutoka kwa mkuu wa wilaya na uongozi wake juu ya
jambo hilo.
Hata hivyo suala hilo kwa upande wa
wananchi liliwalazimu kupaza sauti
wakimtaka mwakilishi huyo kuondoka na watumishi hao ili uongozi wa Manispaa
upeleke timu ya kuwachunguza zaidi akiwemo mkaguzi wa hesabu za ndani kwani
fedha nyingi walihisi zimeliwa.
0 comments:
Post a Comment