Tamko dhidi ya mifuko ya plastiki bado kiporo


Hussein Ndubikile

Magdalena Mtenga
MKURUGENZI Msaidizi wa Mazingira- 0fisi ya Makamu wa Rais, Magdalena Mtenga, amesema mpango mkakati wa Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki uko pale pale na hivi karibuni tamko litatolewa.

Mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba, alitangaza kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ifikapo Januari mosi mwaka huu kutokana na kuchangia uchafuzi wa mazingira, lakini hadi sasa inaendelea kutumika.

Wiki iliyopita, gazeti hili lilimtafuta Waziri Makamba kutaka kujua kwa nini mifuko hiyo inaendelea kutumika akajibu kuwa ndani ya  siku mbili Serikali itatoa tamko hilo lakini halijatolewa.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi huyo alisema msimamo wa Serikali kuzuia matumizi ya mifuko hiyo haujabadilika, huku akisisitiza kuwa suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau ndipo tamko litolewe.

“Suala hili liko palepale kuna mambo yanakamilishwa yakishakamilika tamko linatolewa,” alisema na kuongeza kuwa mchakato wa kupiga marufuku mifuko upo katika hatua za mwisho.

Mbali na Serikali kutoa tamko hilo mwaka jana, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) nalo lilitangaza kupiga marufuku mifuko hiyo baada ya kubaini kuwa kwenye udongo haiozi hivyo kuchangia uchafuzi wa mazingira.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo