Peter Kimath, Morogoro
Peter Lijualikali |
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kilombero imemhukumu Mbunge wa Kilombero,
Peter Lijualikali (30), kifungo cha miezi sita kwa kufanya vurugu na
kusababisha taharuki kwenye mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Mji Mdogo wa Ifakara.
Mwendesha Mashitaka Inspekta wa Polisi, Dotto Ngimbwa
awali alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa namba moja (Peter) na mwenzake
Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi, mwaka jana Kibaoni kwenye
ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Ngimbwa alidai kuwa siku hiyo saa 4 asubuhi Kibaoni
washitakiwa walifanya fujo na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.
Washitakiwa walikana mashitaka na kesi kuanza kusikiliza ushahidi wa pande zote
mbili na upande wa mashitaka kuthibitisha tuhuma bila kuacha shaka.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kilombero, Timothy
Lyon, alisema Mahakama iliwatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshitakiwa wa
kwanza alikuwa na kesi tatu huko nyuma na kutiwa hatiani na kuhukumiwa,
atafungwa miezi sita.
Lyon alitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa
hatiani na kuhukumiwa kuwa ni kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya
mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014.
Alisema Mahakama kwa kuona mshitakiwa ni mzoefu na kuona
katika kesi zote alitiwa hatiani hivyo Mahakama iliona mtuhumiwa ana hatia na
kustahili kutumikia kifungo cha miezi sita jela.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilimwona mshitakiwa wa pili
Stepheno Mgata ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutenda kosa, na hivyo kumhukumu
kifungo cha nje cha miezi sita na ndani ya kipindi hicho hatatakiwa kutenda
kosa lolote la jinai.
Katika hali isiyo ya kawaida Mahakama hiyo ilikuwa tulivu
tofauti na kesi zilizopita ambapo wanachama wachache walijitokeza, licha ya kusambazwa
kwa ujumbe wajitokeze kwa wingi siku ya hukumu.
0 comments:
Post a Comment