Suleiman Msuya
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Edwin Ngonyani, amesema Kivuko cha Mv. Dar es Salaam, kitaanza
kutumika baada ya mkandarasi kukamilisha marekebisho ambayo yanahitajika hasa
kuhusu mwendo wa baharini.
Ngonyani aliyasema hayo jana wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hii aliyetaka kujua sababu za kivuko hicho
kilichoigharimu Serikali zaidi ya sh. bilioni 8 kuegeshwa katika kambi ya Jeshi
la Majini Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kivuko hicho cha MV. Dar es Salaam Kampuni
ya Denmark iitwayo JGH Group (JGH Marine A/S/Johs. Gram-Hanssen A/S) ambapo
baada ya kukamilisha matengenezo ilikabidhi Wakala wa Umeme, Mitambo na Ufundi
(Temesa), lakini imegoma kukipokea kutokana na kuwa na mwendo mdogo.
Alisema kwa sasa kinachoendelea ni
marekebisho hayo ambayo yakikamilika, kivuko hicho kitaanza safari.
Naibu Waziri Nngonyani alisema awali
kivuko hicho kilikuwa kinapaswa kufanya kazi kutoka Dar es Salaam kwenda
Bagamoyo, ila baada ya kukamilika upanuzi wa barabara ya Bagamoyo wanaona
hakitakuwa na tija.
“Kivuko kimesimama kwa sababu kuna
mapungufu ambayo yapo kinyume na mkataba, hivyo yakikamilika kitaanza kazi ila
hakitaenda Bagamoyo,” alisema.
Aidha, alisema wizara ipo katika mkakati
wa kujenga vivuko mbalimbali ambavyo vitatoa huduma katika maeneo tofauti
nchini kama Kilombero, Tanganyika, Nyasa na Victoria.
Naibu Waziri Ngonyani amesisitiza
mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika na ujenzi wa barabara kuepuka kujenga
matuta katika barabara hizo, kwani ni kinyume na utaratibu.
Alisema ni jambo la aibu kuona barabara
zinatengenezwa kwa lami halafu zinawekewa matuta hali ambayo inasababisha
magari kupata matatizo na kutembea mwendo ambao si sahihi.
Alitoa wito kwa wahandisi na wakandarasi
kuhakikisha kuwa wanaweka alama za barabarani pale ambapo kunahitajika kuweka
na si matuta.
Aidha, alisema ni vema presha za kisiasa
kuepukwa katika kujenga barabara kwani inaonekana kuwa sababu ya barabara
nyingi kujengwa kwa kuwekewa matuta.
Halikadhalika Naibu Waziriv Ngonyani
amewataka wanananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa na subira kwani suala la bei
ya kuvuka daraja la Kigamboni linafanyiwa kazi.
0 comments:
Post a Comment