Mashaka Mugeta
Mashaka Mgeta |
UMOJA wa Afrika (AU) umeungana na Watanzania katika
nadharia na vitendo vinavyoelekezwa katika kumkumbuka na kumuenzi Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali
ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza.
Ingawa AU imekuwa ikijikita katika fikra za waasisi wake
na waliopigania uhuru katika mataifa ya Afrika akiwamo Mwalimu Nyerere, lakini
taasisi hiyo iliyoasisiwa kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) imekwenda
mbele zaidi.
Imezindua Kituo cha Amani na Usalama cha Makao Makuu yake
(AU) kilichoitwa Mwalimu Julius Nyerere, kikiwa jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kupewa jina la Mwalimu Nyerere kwa kituo hicho si jambo
jipya, kwa maana yapo majengo, barabara, vyuo, vituo vya maendeleo ya jamii na
vinginevyo katika kona tofauti za dunia hususani barani Afrika, vilivyopewa
jina la Mwalimu Nyerere.
Hivyo hata AU wanapoamua kulitumia jina hilo kwa Kituo
cha Amana na Usalama cha Makao Makuu yake, ni mwendelezo wa hulka na kusudio jema
la kumuweka Mwalimu Nyerere.
Kwamba Mwalimu Nyerere anasimama katika watu wanaopaswa
kuiendeleza misingi aliyoisimamia, ndoto za maendeleo, umiliki wa rasilimali, ujenzi
wa umoja na uwapo wa Amani kwa nchi yake, bara lake na wananchi kwa ujumla.
Kutumika kwa jina la Mwalimu Nyerere ni ishara ya
kukumbuka namna Kiongozi huyo alivyosimamia haki, usawa, kukemea uovu na
kuguswa umasikini wa watu.
Mwalimu Nyerere anapokumbukwa hata na AU, inakuwa rejea
ya kuufikirisha ulimwengu namna ambavyo aliweka kando matendo na fikra zenye kukidhi
manufaa binafsi, familia ama marafiki, bali kuifanya jamii pana ya raia walio
wengi wake wenye furaha.
Kwa maana hiyo, kupitia maisha bora. Mwalimu Nyerere
aliyethamini utu wa mtu, akashiriki kubuni, kutunga na kuzisimamia ahadi 10 za
waliokuwa wanachama wa chama Tanganyika African Nation Union (Tanu) ambacho Februari
5, 1977 kiliungana na chama cha Afro Shiraz cha Zanzibar, kikaanzishwa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Ahadi hizo zenye sifa na viashiria vya tunu za uongozi
bora ni binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja, nitaitumikia nchi yangu
na watu wake wote na nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa
na dhuluma.
Nyingine ni rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa
rushwa, cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo change wala cha mtu mwingine kwa
faida yangu, nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa
faida ya wote.
Pia zikawapo, nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga
nchi yetu, nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko, nitakuwa mwanachama
mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika na ya mwisho ikaandikwa,
nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.
Kwa ufupi, jina la Mwalimu Nyerere linapotajwa na
kumbukumbu ya maisha yake kurejea akilini mwa watu, msingi wake unachagizwa na
ahadi hizo.
Hivi sasa Mwalimu Nyerere hayupo tena duniani katika
umbile lake, isipokuwa fikra zake zipo na zitadumu. Atazidi kuwa rejea ya namna
uongozi wa mataifa hasa ya Afrika unavyopaswa kuwa, hata kama waliopo
madarakani kwa kila nchi, hawawezi kutekeleza, kufuata na kujifunza kutoka kwake.
AU inapofikia hatua ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwa
kulitumia jina lake, lakini ikukumbukwa kwamba Umoja huo ulishakubali na
kuitumia lugha ya Kiswahili iliyotumiwa na mwanasiasa huyo wa karne
kuiunganisha Tanzania na Watanzania, raia wa taifa hili wakiwamo viongozi
wanasimama wapi?
Bila shaka lipo jukumu moja kubwa kwa Tanzania. Jukumu
linapopaswa kuingizwa kwenye mifumo ya kisheria inayotoa adhabu kwa
watakaoikiuka, kwamba misingi iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere inapaswa kuenziwa
ili watu waiishi misingi hiyo.
Misingi iliyo sehemu kubwa ya tunu za Taifa (kama
ilivyowahi kutajwa kwenye rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa na Tume ya Jaji
Warioba) inapaswa kuendelezwa baada ya kuenziwa. Hivyo kuienzi kusiwe
kunakotokana na kauli za kisiasa pasipo utashi na uthubutu unaodhihirika
machoni pa watu.
Tanzania na raia wake wakiwamo waliokabidhiwa na
watakaokabidhiwa dhamana za uongozi, wanapaswa kujiepusha na kuwa mfano wa eneo
la jiografia lenye misitu likakosa wajenzi. Kwamba pamoja na kujaliwa ‘kisima
cha hekima’ za Mwalimu Nyerere, watu waishi ndivyo sivyo!
Mwalimu Nyerere alifundisha kila eneo la kijamii kuanzia
uhusiano wa mtu na mtu, kikundi ama taasisi moja na nyingine, kisha kwa raia
wote. Uhusiano unaojikita katika kuheshimiana, kuvumiliana na kupingana pasipo
kupigana.
Mwalimu Nyerere alielekeza na kufundisha namna bora ya
kuiendeleza misingi ya haki za binadamu na usawa kwa watu wote. Alipinga
unyanyasaji, uonevu na ubaguzi wa kila aina. Kisha akasimamia umoja wa kitaifa
unaochagiza kasi ya maendeleo na ustawi wa watu.
Lakini orodha ya mafundisho na maelekezo ya Mwalimu
Nyerere hayaishi hapo, kwa maana hata yakiandikwa yote si eneo la safu hii ama
gazeti zima litatosha. La hasha, isipokuwa kwa machache yanayotokana na AU ilivyomuenzi
Mwalimu Nyerere.
0754691540
***************************************
0 comments:
Post a Comment