Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta
|
MWISHO wa wiki iliyopita, nilikuwa ninaangalia, kupitia
runinga, hafla ya ufunguzi wa fainali za mashindano ya soka kwa nchi za Africa
(Afcon) yanayoendelea nchini Gabon.
Ufunguzi huo ulitanguliwa na burudani za muziki, miongoni
mwa waliotumbuiza akiwa ni kijana Mtanzania, Nasib Abdul maarufu kama Diamond Plantnumz.
Diamond kama anavyofahamika miongoni mwa wengi, aliagwa
Januari 10, mwaka huu, akikabidhiwa bendera ya Taifa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Wasanii na Michezo, Nape Nnauye.
Tukio la kukabidhiwa bendera halikuwa geni kwangu. Ninaamini
halikuwa geni kwa watu wengi kwa maana imeshatokea na kuzoeleka mara ‘chungu
nzima’, Watanzania kukabidhiwa bendera kama ilivyokuwa kwa Diamond.
Lakini kitendo cha kuonekana kwa bendera hiyo kwenye
ufunguzi wa mashindano ya AFCON kiliibua hisia na kuuona mwanga mpya.
Kwamba kama nchi itadhamiria na kuchukua hatua za
utekelezaji kwa sera mbalimbali zilizopo, mipango na mikakati ya kitaifa ni
dhahiri hakuna jambo la kitaifa, kikanda na kimataifa litakaloshindikana.
Pamoja na kutambua michango yawatu wengine waliowahi
kuliwakilisha Taifa katika matukio tofauti, inapaswa kwa Taifa hususani
wasimamizi na watekelezaji wa sera, mipango na mikakati ya maendeleo katika
nyanja tofauti, kupata jawabu la kuivusha nchi kutoka hapa ilipo.
Imekuwa kawaida kwa wenye mamlaka ya kuyawezesha hayo,
ili kuchagiza kasi ya mafanikio, wanakuwa nyuma, ushindi unapopatikana,
wanajitokeza na ikibidi kwa kujivisha heshima wasiyoistahili.
Mathalani Diamond, akijituma na kuonesha uwezo mkubwa
katika Sanaa ya muziki, jina lake linakua, uwezo wake unaongezeka kama ilivyo
kwa kazi anazozipata iwe kwa kualikwa ama kwa kuomba.
Na anapojituma pasipo kujali ‘upweke’ anaokutana nao
katika safari ngumu zinazompa mfanikio kila uchwao, anabaki kuwa Mtanzania na
kuiwakilisha nchi.
Ndio maana akiwa na wenzake kadhaa, akaiweka Tanzania
katikati ya ulimwengu ulioshuhudia ufunguzi wa mashindano ya Afcon, ingawa timu
ya Taifa (Taifa Stars) haikufuzu mashindano hayo.
Nina hakika, kama Taifa Stars ingefuzu, ni dhahiri kwamba
kungekuwapo Watanzania waliokwenda Gabon kuishangilia na hivyo kuungana na
Diamond na wenzake ‘kuinogesha’ nchi kwenye mashindano hayo.
Lakini kama ilivyo kwa sekta nyingine, michezo imebaki
kudorora licha ya kuwapo sera, mipango na mikakati inayosomeka na kueleweka vizuri.
Tunakwenda wapi?
Hali kama hiyo ipo katika nyanja nyingine za kijamii
hususani zinazolenga maendeleo ya kiuchumi na ustawi katika maisha ya watu.
Jitihada binafsi za raia zimeibua mafanikio dhidi ya
utekelezaji wa mipango, mikakati na sera za pamoja kama taifa. Watanzania wengi
hasa wenye dhamana za usimamizi na utekelezaji wa sera, mikakati na mipango
wamebaki kuwa hodari wa kushangilia mafanikio binafsi badala ya kuwa sehemu ya
kufanikisha mafanikio hayo.
Ndivyo ilivyotokea kwa Diamond mwishoni mwa wiki. Watu
wengi walimshangilia, walishangilia mafanikio yake.
Nina hakika hata watungaji, wasimamizi na watekelezaji wa
sera, mipango na mikakati inayohusu michezo na sanaa, walimshangilia Diamond,
wakashangilia mafanikio yake. Lakini sina hakina kama walipataje ujasiri wa kuzihoji
nafsi zao, “nimechangia nini katika hili?
Ama kama ningetimiza wajibu wangu, tungefikia ukomo gani
wa kushangilia zaidi ya huu unaoishia kwa ‘mwalikwa’ Diamond?
Tukiuacha mfano huo, hivi sasa Serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais John Magufuli ipo katika mpango wa kuifanya nchi kuwa yenye
uchumi unaotegemea viwanda.
Uchumi wa viwanda ni dhana pana. Hata tafsiri ya viwanda
vidogo vinavyodaiwa kuchochea ukuaji wa uchumi kwa raia na kutengeneza ajira
nyingi bado ‘inapindishwa’ hususani na wanasiasa.
Je, wenye dhamana kwa kila eneo husika wamejiandaa vipi
kuitazama Tanzania, wakilenga ubunifu, ujuzi, taaluma, uzoefu na aina yoyote ya
mchango utakaoifanya nchi kuwa ya viwanda?
Ama kama inavyoonekana sasa kwa Diamond, watu wataendelea
kubweteka, washindwe kutimiza wajibu wao wakisubiri wachache ‘watakaotoka’ kwa
mafanikio, basi tuungane kuwashangilia.
Pamoja na dhamira yake nzuri, Rais Magufuli pekee hawezi
kuifanya Tanzania kufanikiwa katika sekta ya viwanda. Kwa maana ili viwanda
viwepo, vikiwategemea na kuwanufaisha raia wa Tanzania, yapo mambo mengi yanayopaswa
kufanyika.
Miongoni mwa hayo ni kuwasomesha na kuwaandaa wataalamu
wa kuendesha ama kukarabati viwanda, wajuzi wa vipuri, wasambazaji wa malighafi
za uzalishaji hususani mazao ya kilimo, watunzaji na wengine kedekede.
Sera za uchumi zipo, mipango na mikakati inayolisukuma
gurudumu la sekta hiyo ipo, wasimamizi wake wake, je wanafanya nini sasa hivi
kwa ajili ya Tanzania na Watanzania?
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, alipenda kutumia msemo
mmoja wakati akihimiza jambo jema, kwamba “hili linawezekana ikiwa kila mmoja
atatimiza wajibu wake.”
Hata sasa, maana ya usemi wa Rais mstaafu Kikwete maarufu
kama JK bado ‘inaishi’ katikati ya maisha ya watu.
Pasipo kutimiza wajibu, watu wengi wataendelea kuwa
washangiliaji wa mafanikio yanayofikiwa na wachache. Hapo taifa halitapiga
hatua ya maendeleo. Ni muhimu Taifa likajikita katika utekelezaji wa sera,
mipango na mipango ya maendeleo kwa vitendo.
0754691540
0 comments:
Post a Comment