Mwandishi Wetu, Kahama
Dk. John Magufuli |
WAZIRI Mkuu wa
zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amesema CCM inatiwa
kiwewe na kasi ya kuimarika kwa umoja na mshikamano wa vyama upinzani nchini.
Lowassa alitoa
kauli hiyo jana alipozungumza mjini hapa akiwa njiani kuelekea Kagera kwa ziara
ya kuimarisha chama.
Alisema kuimarika
kwa mshikamano huo chini ya mwavuli wa UKAWA ni hatua kubwa katika kuelekea
kuing'oa CCM madarakani.
“Wameanza mbinu
za kutaka kutuondoa kwenye umoja wetu, wameanza kuwalisha viongozi wetu maneno,
mfano gazeti… la Januari 12 walinilisha maneno kwamba eti nimeitabiria CCM
ushindi katika uchaguzi mdogo wa udiwani Arumeru...hayo ni mambo ya ajabu
kabisa, gazeti linaamua kutumika kuvunja demokrasia? Inasikitisha sana,”
alisema Lowassa.
Lowassa aliyefuatana
na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema wananchi
wameshajua mbinu chafu za CCM na hawako tayari kuona hamu yao ya mabadiliko
inapotea.
Alisema viongozi
wa vyama vya upinzani wako kwenye mshikamano mkubwa na kuwataka wanachama kuiga
mfano huo.
“Katika ziara
zetu hizi za kuimarisha chama pia tunaimarisha mshikamano miongoni mwetu wapinzani.
CCM wanapata kiwewe na tunawaambia hata wafanyeje, mabadiliko hayaepukiki,
watawatia ndani viongozi wetu kwa hila, lakini wajue hiyo ndiyo inazidisha
vuguvugu, huu ni upepo unaovuma kote duniani hivi sasa wajifunze yaliyotokea
Gambia, Ghana na kwingineko,” alisema Lowassa.
Lowassa na
msafara wake walisalimiana na wananchi kwenye mnada wa Lusaunga, Biharamulo
ambako wananchi hao walimwambia kuwa hali yao ya maisha ni ngumu kutokana na
ukame unaowakabili.
Hata hivyo,
Lowassa hakusema lolote zaidi ya kuwapungia na kuwasalimia akisema mikutano ya
hadhara imepigwa marufuku na asingependa kuvunja sheria na amri hiyo hata kama
ni kandamizi.
0 comments:
Post a Comment