Charles James na Celina Mathew
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amekemea vyombo vya habari
vinavyoandika uchochezi hasa magazeti aliyotaja kuwa yako mawili, huku akisisitiza
kuwa siku zao zinahesabika.
Kauli hiyo aliitoa mjini Shinyanga jana wakati akizindua
kiwanda cha chakula cha Jambo Food Product, kinachomilikiwa na Mbunge wa Meatu,
Salum Mbuzi, ambapo alisema kwa kiasi kikubwa magazeti hayo yamekuwa yakigeuza
habari na kuandika uchochezi jambo
linalohatarisha amani ya nchi.
“Serikali ya kutumbua
majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi,
hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi,
chini ya utawala wangu hilo halitakuwepo.
“Kuna magazeti mawili tu
kila ukisoma wao ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii, wao wanageuza hii,
nasema nataka wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia
wasisikie lakini magazeti mengine na vyombo vyote vingine vinatoa uchambuzi
mzuri sana,” alisema.
Akitolea mfano namna vyombo vya habari vilivyohatarisha
amani ya nchi, Rais Magufuli alisema mauaji ya Rwanda kwa kiasi kikubwa
yalichochewa na wanahabari waliosababisha vifo vya mamilioni ya watu.
"Kuna nchi jirani (ambayo hakuitaja), watu walikufa
kutokana na hao hao wanahabari waliokuwa wanaandika habari za kichochezi,
naomba watambue kuwa hapa nchini sitakuwa tayari kuona amani inachezewa,"
alisisitiza.
Alisema kwenye utawala wake hatakubali kuifanya Tanzania
kuwa nchi isiyo na amani kwa ajili ya vyombo vichache vya habari vinavyotumiwa
na wanasiasa kuvuruga amani.
"Kwenye utawala wangu sitakubali kuona nchi
inapoteza amani yake kwa ajili ya vyombo vichache vinavyotumiwa na wanasiasa,
kwa kuwa hata Wakiristo kwenye maandiko kuna maneno wanayosema kuwa amani nawaachieni
hivyo tutambue kuwa amani hainunuliwi, tuilinde," alisema.
Rais Magufuli alitaka vyombo vilivyobaki kutoandika
habari za kichochezi kwa kuwa vinafanya kazi kwa weledi wa hali ya juu, viendelee
hivyo hivyo.
Kuhusu kiwandi hicho kinachotengeneza bidhaa mbalimbali
za vyakula na vinywaji, Rais Magufuli alimpongeza Mbunge huyo kwa kumsifu kuwa amemuanzishia
mwaka vizuri.
Rais Magufuli alisisitiza kuhusu azma yake ya kuwa na
Tanzania ya viwanda ikiwa na lengo la kuimarisha uchumi na kutoa ajira kwa idadi
kubwa ya wananchi.
Alimsifu Mbuzi kwa uzalendo aliouonesha wa kuanzisha
kiwanda katika ardhi ya nyumbani kwake, ambapo licha ya kukuza pato la Taifa
lakini pia ametoa idadi kubwa ya ajira kwa Watanzania wenzake, huku akitoa wito
kwa wawekezaji wengine kuchukua mfano wa mbunge huyo.
“Nakaukiwa maneno ya kuongea kutokana na hiki
nilichokiona hapa, nimepita kukagua na kujionea ubora wa kiwanda pamoja na
kushuhudia uzalishaji wa kisasa ambao ni nadra sana kuonekana katika nchi za
Kiafrika, hakika Mbuzi ninakusifu na ninaahidi kukupa ushirikiano wa dhati.
“Nikiwa na watu kama ninyi naamini lengo la Tanzania ya
viwanda niliyoihubiri katika kampeni zangu litatimia, tayari kule Pwani viwanda
48 vimeshaanzishwa na jana nimefungua kiwanda kingine cha utengenezaji wa chaki
kule Meatu, hii ni kuonesha jinsi gani kazi inafanyika,” alisema Rais Magufuli.
Aliwapongeza viongozi wa mkoa kwa namna ambavyo wamekuwa
wakipambana kuhakikisha wanajenga Shinyanga ya viwanda na kuwataka kuharakisha
kufufua kiwanda cha nyama, ambacho mwekezaji wake ameshindwa kukiendesha kwa
muda mrefu bila kuwa na sababu ya msingi.
“Tunahitaji wawekezaji wazalendo kama Mbuzi, siyo wale
wengine ambao fedha zao wanaenda kuzificha nje ya nchi na wakifa zinapotelea
huko huko, nikusifu wewe kwa kutoa ajira kwa Watanzania wenzako lakini kama
haitoshi hata bei ya vinywaji vyako naambiwa ni rahisi,” alisema.
Alimtaka Mbuzi kuhakikisha anajali maslahi ya wafanyakazi
wake kwa kuwalipa mishahara mizuri huku akimtoa wasiwasi kuwa yale yote yanayohihusu
Serikali amuachie na hata suala la kodi anaweza kuangalia jinsi gani ya
kumpunguzia.
0 comments:
Post a Comment