IDARA ya Habari, Maelezo imemkabidhi kwa
Jeshi la Polisi mkazi wa Dar es Salaam Joseph Sheka, anayemiliki kampuni ya
Fukanu kwa tuhuma za kuwasilisha nyaraka za kughushi kwa nia ya kuitapeli
Serikali ili kusajili gazeti.
Tukio hilo ambalo lilitokea jana saa
saba mchana lilishuhudiwa gari ya Jeshi la Polisi likifika idarani hapo na
kuwakamata watu wawili, mmoja akiwa ndiye Sheka ambaye alitarajiwa kuwa Mhariri
wa Gazeti hilo.
Akizungumza jana Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara hiyo, Dk Hassan Abbas ambaye hakuweka wazi walitumia njia
gani ili kuwakamata, alisema mtuhumiwa huyo alifikisha nyaraka hizo idarani
hapo akitaka kusajili gazeti liitwalo Lete Mambo.
Alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa
katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano
zaidi ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
"Anatuhumiwa kuwasilisha nyaraka
mbalimbali akidai kuwa ni za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo uchunguzi
wa awali ulibaini kuwa alighushi mihuri na saini za maofisa wa Mamlaka hiyo,
ili kufanikisha azma yake," alisema.
Aidha, alisema taasisi za kiserikali huwa
makini katika kipindi kama hiki kwa matukio hayo yanayoonekana kuwa makubwa.
Hata hivyo, aliiasa jamii kuwa huu si
wakati wa kujaribu kuishi kwa njia zisizo halali na badala yake kufuata
taratibu halali mtu anapotaka huduma katika maeneo mbalimbali ya ofisi za umma.
"Bila kuathiri uchunguzi unaondelea
na utakaotolewa taarifa zaidi na Polisi naomba nitoe rai kwa ofisi za umma kuwa
makini na nyaraka zinazowasilishwa kwao, kwani zingine ni kwa ajili ya kuitia
hasara Serikali,” alisema Dk Abbas.
0 comments:
Post a Comment