Ibrahim Yassin, Mbeya
MIEZI michache imepita jamii haijasahau
tukio la walimu wa sekondari ya Mbeya kumdhalilisha mwanafunzi, tukio linalokaribiana
na hilo limetokea kwenye sekondari ya Ihanga jijini hapa kwa mwanafunzi wa kidato
cha pili, Caleb Mwita kuchaniwa suruali na kutembezwa uchi madarasa yote
akizomewa na wanafunzi.
Akisimulia tukio hilo jana, mzazi wa
mwanafunzi huyo, Joseph Mwita wa Soweto jijijni hapa, alisema lilitokea
mwishoni mwa wiki baada ya kijana huyo kuvaa suruali isiyotakiwa siku hiyo shuleni
ndipo Mwalimu Mapunda alipomwadhibu kwa kumchapa viboko tisa.
Kama haitoshi, Mwalimu Bathlomew Kibona
alimchania suruali hiyo ikidaiwa haiendani na sare za shule hivyo alimvua mwanafunzi
viatu akaichana na kumwacha viungo vikionekana na kumtembeza madarasani kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha nne huku wanafunzi wa jinsi zote wakishuhudia.
Mkuu wa Shule, Theresia Mwaifwani alikiri
kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema Mratibu wa Elimu Kata ndiye mwenye jukumu
la kulizungumzia.
Mratibu, Magdeni Sindika naye alikiri kuwapo
tukio hilo na kusema mwanafunzi Caleb alikiuka kanuni za shule.
Aidha, Sindika alisema adhabu ya walimu
hao ilikuwa kubwa kwa mujibu wa sheria na watajadiliana na Ofisa Elimu wa Jiji,
ili kuona adhabu wanayostahili walimu hao na kumwomba mzazi awasamehe kwa walilofanya
na kuahidi kumtafutia shule nyingine mwanafunzi huyo ili asome bila fadheha.
Mzazi Mwita alisema hapingi adhabu ya
walimu hao lakini kitendo cha kuchaniwa suruali na kudhalilishwa kwa wanafunzi
wenziwe hali na kumfanya kijana wake aathirike kisaikolojia hakikubaliki.
Caleb alisema suruali aliyovaa ni ya
shule isipokuwa siku hiyo alivaa nyeusi badala ya kahawia na haikuwa inabana
kama ilivyodaiwa na walimu na pia adhabu ya viboko ilitosha na si kuchaniwa
suruali na kutembezwa madarasani akiwa uchi.
Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa, Protas
Mpogole alikiri kupata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo na
kwamba Halmashauri ya Jiji Kitengo cha
Elimu inashughulika suala hilo.
0 comments:
Post a Comment