Hussein Ndubikile
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu nchini (HESLB) imesema inaendelea na uchambuzi wa majina yaliyowasilishwa
na waajiri ili kubaini waajiriwa wanufaika wanaotakiwa kurejesha fedha za
mikopo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bodi hiyo
kufanya msako wa ofisi kwa ofisi katika kampuni za Dar es Salaam na kuagiza
waajiri wote kuwasilisha majina ya waajiriwa iweze kubaini wanaokwepa
kurejesha.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Meneja
Urejeshaji Mikopo wa Bodi hiyo, Deodatus Mwiliko alisema baada ya msako huo na
kuagiza waajiri walete majina ya waajiriwa wao kwenye ofisi za HESLB
walitekeleza na kinachofanyika sasa ni uchambuzi wa kina kubaini wanufaika.
“Tunaendelea na uchambuzi wa majina ya
wanufaika yaliyoletwa na waajiri tukishamaliza kuchambua tutawakata makato kama
sheria za Bodi zinavyoelekeza,” alisema.
Alisema Bodi ilikagua kampuni 24 na
kubaini kasoro zikiwamo za kutowasilisha majina ya waajiriwa, kuwasilisha
makato pungufu nje ya muda na waajiri kutofahamu sheria za Bodi.
Alizitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni
shirika la ndege la Precison Air, Pepsi, Jambo Plastics, Jumbo Plastics,
Sadolin na Tanzania Printers Ltd.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi
hiyo, Abdul-Razaq Badru wanufaika walio kwenye ajira rasmi wanatakiwa kukatwa
asilimia 15 ya mishahara yao na ambao hawako kwenye ajira isiyo rasmi watakatwa
asilimia 10 ya kipato wanachopata kwa mwezi.
0 comments:
Post a Comment