*Wanasheria wasema uteuzi wao wapingana na Katiba
*Kifungu chasisitiza idadi ya angalau
wanawake watano
Fidelis Butahe
Profesa Palamagamba Kabudi |
NANI atatoswa? Ndilo swali la kujiuliza
kutokana na ubunge wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo
na nguli wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi wanaosubiri kuapishwa baada ya
kuteuliwa na Rais John Magufuli, kuwa shakani kutokana na uteuzi wao kutoendana
na Katiba.
Bulembo na Kabudi waliteuliwa Jumanne kuwa
wabunge na hivyo kusubiri kuapishwa katika Mkutano wa Sita wa Bunge utakaoanza Januari
31 mwaka huu, lakini kabla ya kuapishwa, imebainika kuwa uteuzi wa mmoja wao unapingana
na Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu hicho cha Katiba kinasema uteuzi
wa Rais wa nafasi 10 za wabunge, angalau watano wanapaswa kuwa wanawake.
“Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na
Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya ya (a) na (c) za uibara ya 67 na
angalau wabunge watano kati yao wakiwa wanawake,” inasema Ibara hiyo ya Katiba
ya mwaka 1977.
Kutokana na kifungu hicho wanasheria waliozungumza
na gazeti hili walisema kuapishwa kwa Bulembo na Profesa Kabudi, kutakiuka
kifungu hicho cha Katiba kwa sababu mpaka sasa Rais ameteua wabunge wanane,
huku wawili tu wakiwa ndio wanawake huku zikiwa zimebaki nafasi mbili za
uteuzi.
Walisema kutokana na masharti hayo ya
Katiba, hata akiteua wanawake katika nafasi hizo mbili, bado hawatafikia
watano, na kusisitiza kuwa uapisho wa mmoja wa wateule hao au wote, utapaswa
kusitishwa ili kulinda kiapo cha Rais, Spika wa Bunge na Katibu wa Bunge cha
kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Walisema mbali na kuwa kinyume na Katiba,
huenda kuapishwa kwao bungeni kukazua mvutano mkali kutoka kwa wabunge, kwa
sababu wawakilishi hao wa wananchi watatumia Katiba ya nchi kupinga jambo hilo.
Tayari Baraza la Wanawake Chadema
(Bawacha) limeibuka na kueleza kusudio la kufungua kesi mahakamani kwa hati ya
dharura, kupinga uteuzi huo, kwa sababu ni kinyume na Katiba, likiitaka Mahakama
itoe tafsiri ya kisheria.
Wateule
Tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka
juzi, Rais Magufuli ameshateua wabunge wanane, wakiwamo Bulembo na Profesa
Kabudi.
Wawili ni wanawake ambao ni Naibu Spika
wa Bunge, Dk Tulia Ackson na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino
Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Dk Philip
Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi
ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.
Wanasheria
Kwa masharti ya kutotajwa gazetini kwa
maelezo kuwa wateule hao ni watu wake wa karibu, mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria alisema:
“Katiba inasema wasiteuliwe wanaume
zaidi ya watano, maana yake angeweza kuteua wanawake hata saba na wanaume
watatu. Wanaume hawapaswi kuzidi watano, ila wanawake wanaweza hata kuzidi
watano.”
Alisema wateule hao watakapoapishwa
bungeni, wabunge wanaweza kuwasilisha hoja ya kutaka wasiapishwe, ili uteuzi
huo urejeshwe kwa Rais sambamba na tamko kuwa kiongozi mkuu wa nchi amekiuka
Katiba, lengo likiwa ni kumtaka apitie upya uteuzi huo.
“Nadhani ndicho kitakachofanyika. Hapo
ni wazi kuwa Rais amevunja Katiba. Wakienda kuapishwa, Mbunge mmoja anaweza
kuibua hoja ya kuvunjwa kwa Katiba, ili Spika atoe uamuzi wa kurejesha majina
ya wateule hao kwa Rais na kumshauri kuwa Katiba hampi mamlaka ya kuteua
wanaume zaidi ya watano,” alisisitiza msomi huo mwenye Shahada ya Uzamivu.
Huku akielezea maana ya wabunge
wasiozidi kumi, angalau watano kati yao wakiwa wanawake, alisema, “Rais
angeweza kuteua wanawake wanane na wanaume wawili lakini si wanawake
chini ya watano.”
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk
James Jesse alisema: “Inavyoonekana Rais hakutazama hicho kifungu, nadhani hilo
ndio kosa lililofanyika. Hicho kifungu kiko sawa, kinasema angalau wanawake
watano, maana yake wanawake wasipungue watano.”
“Kama ikiachwa hivi kutakuwa na uvunjifu
wa Katiba, vinginevyo kama ikibainika hivyo ashauriwe vinginevyo, kama kuna
ambao atawapunguza. Hapo ndipo inapotakiwa washauri wa Rais wafanye kazi kwa
kutazama sheria kila wakati, lakini wakijisahau mambo kama haya hujitokeza.”
Serikali
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alisema: “Huo ni
mjadala uendelee tu. Katika mjadala watu hawazuiwi kujadili, binafsi sipo kwenye
mjadala huo. Waache wajadili ufafanuzi kuhusu mjadala hilo utatolewa wakati ukifika. Huwezi kuzuia
watu kujadili.”
Chadema
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alisema: “Hilo jambo mbona Katiba imeweka wazi. Sijui Spika atafanyaje siku ya
kuapisha, maana uteuzi ni kinyume na Katiba. Tutaomba Mwongozo bungeni kuhusu
suala hili, hatutanyamaza.”
Wakati Lissu akieleza hayo, Mwenyekiti
wa Bavicha na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema: “Tutakwenda mahakamani
kupinga uteuzi huu, licha ya kujua kuwa Katiba iko wazi.
“Unapokuwa na neno ‘angalau’ tafsiri
yake ni wasiwe chini ya watano, ila wanaweza kuwa zaidi ya hapo. Hadi sasa Rais
ameteua robo tatu, hata hao waliobaki wawili, akiteua wanawake atakuwa amekiuka
matakwa ya kikatiba, maana watakuwa hawafiki watano,” alisema Mdee.
Mdee alisema suala hilo si la wanawake
wa Chadema pekee, linapaswa kupigiwa kelele na taasisi zingine kwa ajili ya
kutetea wanawake.
Nani kunusurika?
Mapema baada ya uteuzi wa wabunge hao,
wasomi na wataalamu wa siasa na utawala, walimzungumzia Profesa Kabudi kuwa
uteuzi wake si wa kujaza viti vya ubunge pekee, bali umelenga kujaza moja ya
viti kwenye Baraza la Mawaziri.
Mmoja wa wasomi hao, Dk Benson Bana wa UDSM
alisema: “Siwezi kuwa mtabiri lakini ukisoma alama za nyakati na uteuzi huu
kufanyika sasa, inawezekana si wote lakini nafikiri anaweza (Rais) kufanya
mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri.
“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi
na anaijua Tanzania. Ana uwezo mkubwa, wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani
kama Rais atamwacha tu hivi hivi awe mbunge tu.”
Alisema Bulembo anaweza asiteuliwe kuwa
waziri, lakini akatumika ndani ya Bunge kuimarisha umoja wa wabunge wa CCM.
Kikwete
Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika
muhula wake wa pili wa utawala, aliteua wabunge 10 na kati yao watano walikuwa wanawake.
Alimteua Zakhia Meghji na alipofanya
mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwaka 2012, aliwateua Janet Mbene na Saada
Mkuya na kuwateua kuwa naibu mawaziri Wizara ya Fedha.
Aidha, akamteua Dk Asha-Rose Migiro kuwa
Waziri wa Katiba na Sheria na wakati anakaribia kuondoka madarakani, akamteua
Dk Grace Puja.
0 comments:
Post a Comment