*Asema siku si nyingi atakuwa Rais
Fidelis Butahe
Maalim Seif Sharif Hamad |
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Sharif Hamad, amedai kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
inamnyanyasa, huku akisisitiza kuwa naye pia siku si nyingi atakuwa Rais.
Mbali na kauli hiyo aliyoitoa jana
kupitia Kipindi cha Funguka kilichorushwa na Televisheni ya Azam, Seif alitaja
mambo 12 yanayohusu mustakabali wake kisiasa na kufafanua mambo kadhaa
yanayohusu mgogoro unaoendelea ndani ya CUF.
Katika kipindi hicho, Seif ambaye
aligombea urais Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 ambao
ulifutwa na kurudiwa Machi 20, mwaka jana, aliulizwa takriban maswali 15 na
mwongozaji wa kipindi hicho, Tido Mhando.
Maalim Seif alizungumzia kuhusu matibabu
yake, baada ya kumaliza muda wake na kubainisha kuwa ameamua kujigharamia
kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kile alichoita uwezekano wa kunyanyaswa.
“Safari zangu zote za matibabu najilipia
mwenyewe siombi serikalini. Siombi kwa sababu ukiwaambia wanakuwa na
manyanyaso,” alieleza Seif na kuongeza;
“Nikasema nitajipeleka mwenyewe,
matibabu yote ninayokwenda baada ya wadhifa wangu najilipia mwenyewe ingawa
nina haki kikatiba ya kulipiwa.”
Seif alienda mbali na kutaja haki anazopata
sasa kutoka serikalini akiwa kiongozi mstaafu kuwa ni kutumia gari la Serikali,
mlinzi na kulipwa posho.
“Nilikuwa Makamu kwa Kwanza wa Rais,
baada ya kustaafu kuna haki ambayo lazima nipate, wala hawafanyi hisani ni haki
yangu,” alisema na kuzitaja haki hizo.
Akijibu swali lililomtaka aeleze kama
bado anaota kuwa rais wa Zanzibar, Seif alijibu “tena si mbali, natarajia muda mfupi ujao inshallah nitakuwa
rais wa Zanzibar.”
Awali, akisisitiza kuhusu kuwania nafasi
hiyo alisema, “ngoja tupate haki yetu (mahakamani) na mimi nikawa rais wa
kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hapo ndio tutaona serikali ijayo
itakuwaje.”
“Kwanza tuone tunafanikiwa au
hatutafanikiwa ila baada ya hapo ninaweza kufanya maamuzi. Sasa ninajua
tutafanikiwa. Kugombea 2020 ni jambo ambalo ni lazima, tusubiri muda ufike tuone na hali ya kisiasa.
CUF haijadhoofika.”
Seif amegombea urais Zanzibar mwaka
1995, 2000, 2005, 2010, huku mwaka 2015 ndoto zake zikiyeyuka baada uchaguzi
kufutwa kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Jecha aliitangaza Machi 20, mwaka jana
kuwa siku ya marudio ya uchaguzi huo ambao ulisusiwa na CUF kwa sababu ni
kinyume na sheria na Katiba jambo lililoipa mwanya CCM kuibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 95.
Katika kipindi hicho cha saa moja,
Maalim Seif alizungumzia mgogoro wa CUF ulioibuka baada ya mwenyekiti wa chama
hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kutambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, kusisitiza kuwa msomi huyo alipojiuzulu taratibu zilifuatwa, hawezi
kupewa nafasi nyingine.
Mambo mengine aliyoyazungumzia ni kesi
zilizopo mahakamani, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kujiunga Ukawa,
Lipumba kutumiwa na dola, uchaguzi mdogo, kasoro uchaguzi wa ubunge jimbo la
Dimani Zanzibar sambamba na Uchaguzi Mkuu uliopita.
Nyingine ni maridhiano Zanzibar,
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ruzuku ya chama hicho pamoja na jinsi
anavyozunguzwa katika kulipiwa fedha za matibabu licha ya kuwa alikuwa Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Mgogoro CUF
Akizungumzia mgogoro CUF alisema kundi
linaloongozwa na Profesa Lipumba ndio linalozua tafrani katika chama hicho huku
wakisaidiwa na Ofisi ya Msajili.
“Tulimsihi Lipumba asijiuzulu, lakini
alishikilia msimamo wake. Hakufukuzwa alijiuzulu mwenyewe na baada ya miezi 10
anaandika barua kwamba anatengua uamuzi wake, jambo hili sijawahi kuliona
duniani,” alisema.
Huku akieleza jinsi CUF kilivyoshindwa
kukutana kwa wakati muafaka kupitia mkutano mkuu wake kujadili barua ya Lipumba
kujiuzulu kwa sababu ya kukabiliwa na ukata, Maalim Seif alisema mkutano huo
ulifanyika baadaye na uamuzi ukatolewa kwa kufuata Katiba ya chama hicho.
“Hatukubaliani na msajili ndio maana
tumefungua kesi Mahakama kuu ili tupate tafsiri ya uamuzi huu. Msajili hawezi
kutengua uamuzi wa kikao halali cha chama, hatukuridhika na uamuzi wake,”
alisema.
Alisema iwapo CUF kitashindwa katika
kesi hiyo watakubaliana na uamuzi huo licha ya kuwa watakuwa na nafasi ya
kukata rufaa katika Mahakama ya rufaa.
Akijibu hoja zilizowahi kutolewa na
Lipumba kuwa alijizulu baada ya kuchukizwa na kitendo cha Ukawa kukubali
Lowassa agombee urais alisema, “Lipumba
hana msimamo. Yeye ndio aliyemleta Lowassa, akasema akija kwetu atatusaidia na
tulikubaliana Lowassa atakuwa mgombea wetu hapo ndio akabadilika.”
“Hana nia njema alidhani akijiuzulu watu
wengi watamfuata ila haikuwa hivyo. CUF bila Lipumba huku ikishirikiana na
Ukawa imefanya vizuri zaidi, imeshinda majimbo 10 Tanzania Bara. Tulipata
Halmashauri za wilaya nne na nyingine tano kwa kushirikiana na wenzetu wa
Ukawa.”
Alisema katika katika uchaguzi mdogo
uliofanyika wiki iliyopita Lipumba alisimamisha wagombea katika kata 11 na
kushindwa huku wagombea wakipata kura kati ya 10 hadi 15.
Maridhiano
“CCM hawakubali matokeo ya Oktoba 2015
ambayo yalifutwa kinyume na sheria na taratibu, sisi hatukubali matokeo ya
Machi 20 mwaka jana kwa sababu yalifanyika kinyume na Katiba. Hapo lazima
tutafute njia ya kutoka na lazima tuzungumze na upande wa pili,” alisema.
Akizungumzia jinsi walivyokutana na Rais
mstaafu Zanzibar, Aman Abeid Karume na kukubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK), alisema lengo lilikuwa ni kuwafanya wananchi kuwa kitu kimoja na
ndio ukawa msingi wa kufanyika kwa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.
“Inawezekana kwa sasa tukarejesha SUK kama
kutakuwa na nia njema kwa kila upande ukubali Zanzibar kuna tatizo na haja ya
viongozi kupata ufumbuzi wa matatizo ili kushirikiana pamoja. Miaka mitano
iliyopita mambo yalikwenda vizuri ila kwa sasa ugomvi na uhasama umerudi.
Hakuna dawa Zanzibar isipokuwa vyama kushirikiana,” alisema.
Ruzuku
Kuhusu Ofisi ya Msajili kutoa ruzuku kwa
kundi la Profesa Lipumba alisema, “nilimuandikia barua kuhoji sababu za
kutopewa ruzuku akanijibu kwamba kazuia ruzuku kwa sababu chama kina mgogoro
cha ajabu akaruhusu upande wa Lipumba upate ruzuku.”
Alisema fedha hizo zimekwenda katika
akaunti ambayo yeye haijui wala Bodi ya Wadhamini ya chama hicho na huku
akihoji jinsi ukaguzi wa fedha hizo utakavyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG).
“Hata mimi Msajili ananitambua, iweje
fedha ampe mwenyekiti asiyehusika na masuala ya fedha. fedha hizi zitakaguliwa
vipi? Fedha za chama zilikuwa zinakwenda kwenye akaunti inayotambulika si
akaunti mpya,” alisisitiza.
Alisema wamemuandikia barua Msajili,
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), kwamba wanatarajia kufungua kesi kupinga jambo hilo.
0 comments:
Post a Comment