Suleiman Msuya
Jecha Salim Jecha |
BAADA ya kimya cha muda mrefu Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amevunja ukimya akieleza
kuwa tangu Mapinduzi ya Zanzibar, nchi hiyo haijawahi kufanya uchaguzi usio na
misuguano.
Aidha, amesema asingetaka kuzungumzia uamuzi
wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka juzi kwa kuwa hilo lina historia
ndefu na angependa kwanza ikamilike ripoti ya mchakato wa uchaguzi huo.
Jecha alisema hayo alipokuwa akizungumza
kupitia Kipindi cha Funguka kilichorushwa na Kituo cha Azam kikiongozwa na
mwandishi mkongwe nchini, Tido Mhando.
“Historia inaonesha kuwa Zanzibar tangu
Mapinduzi hatujawahi kufanya uchaguzi ukaisha kwa amani, hivyo ni jambo ambalo
linapaswa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa dhana hiyo inaondoka,” alisema.
Alisema katika uchaguzi wa Oktoba 25
mwaka 2015 mchakato wa kupiga kura ulienda vizuri, ila tatizo lilikuja wakati
wa majumisho.
“Kusema kweli uchaguzi ulifanyika vizuri
ila kulikuwa na dosari mbalimbali ambazo zililalamikiwa na baadhi ya vyama vya
siasa, hivyo nililazimika kufanya nililichokifanya pamoja na kuonekana peke
yangu ila ni maamuzi ya ZEC,” alisema.
Alisema kwenye Tume mgawanyiko unaweza
kutokea hasa ukizingatia mfumo wa Tume ya Zanzibar ambayo inashirikisha vyama.
Mwenyekiti huyo alisema changamoto kubwa
katika uchaguzi wa mwaka 2015 zilionekana katika upande wa Pemba ambako
watendaji walionekana kukiuka baadhi ya taratibu.
“Wakati matokeo ya Unguja yanaingia
hakukuwa na matatizo, ila yalipoanza kuingia matokeo ya Pemba tulianza kuona
ukiukwaji wa taratibu hasa katika masuala ya kiufundi, hakukutokea vurugu,
lakini kulitokea mapungufu yaliyonisukuma kufanya nilichofanya,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kasoro hizo
za matokeo ya uchaguzi Zanzibar, hazijaonekana kwa upande wa wagombea wa
Muungano kwa sababu hisia za uchaguzi zipo upande wa Zanzibar.
Alisema viongozi wa kisiasa na wananchi
katika kisiwa hicho wamejawa na jazba za kisiasa hali ambayo inachangia kuwepo
kwa mtafaruku.
Kwa nini alifuta matokeo?
Kuhusu sababu za kufuta matokeo, alisema
ataziainisha katika ripoti hiyo, ambayo imebainisha kila kitu huku akisisitiza
kuwa utaratibu ulifuatwa katika uamuzi huo.
Jecha alikanusha taarifa kuwa uamuzi huo
wa kufuta matokeo ulitokana na maagizo ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, huku
akisisitiza kuwa hata namba yake ya simu hana.
Alisema historia inaonesha kuwa uchaguzi
Zanzibar umeshafutwa, hivyo isionekane jambo jipya na kubainisha kuwa iwapo
kutakuwepo na mfumo bora zaidi yeye yupo tayari kufanya nao kazi kwa maslahi ya
Zanzibar na Wazanzibari.
Mwenyekiti huyo alisema katika uamuzi
wake hakupendelea chama chochote, ila alifuata taratibu na kama angependelea
angeweza kutangaza ushindi na si kurudiwa kwa uchaguzi.
“Ukiwa kiongozi kuna wakati unalazimika
kuchukua maamuzi mazito, kwani huwezi kuona jahazi inazama unaacha kuchukua
maamuzi kisa kusubiri watu wafanye uamuzi huku wengine wakifa,” alisema.
“Narudia kama kiongozi ukikabidhiwa
jambo lolote si lazima usubiri maamuzi ya vikao unatakiwa kuchukua hatua na
ndivyo nilivyofanya,” alisema.
Amzungumzia Maalim Seif
Jecha pia alisema kitendo cha aliyekuwa
mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza matokeo hayo kilikuwa
kinyume na sheria na taratibu.
Alisema matokeo ambayo Hamad alitangaza
yalikuwa batili, hayakuwa sahihi yalikuwa yamepikwa na yalikiuka taratibu hivyo
kuvitaka vyombo husika kufanyia kazi na si tume.
“ZEC haikumuonea Seif ila mambo ambayo
yalifanyika hayakuwa sahihi ni ngumu kuvumilika,” alisema
Ilivyokuwa Oktoba 28, 2015
Jecha alisema kuwa uchaguzi huo haukuwa
wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi.
Alisema baadhi ya makamishna wa tume
hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni
wawakilishi wa vyama vyao".
"Kumegundulika kasoro nyingi katika
uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba
vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika."
Alisema hilo ni jambo la kushangaza
ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapigakura hawakwenda kuchukua vitambulisho
vyao vya kupigia kura".
Kadhalika, alisema kura hazikupata
ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba ambako alisema kuwa baadhi ya mawakala wa
baadhi ya vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.
Aliongezea kuwa vijana katika eneo hilo
walivamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kutaka kuzua ghasia, na pia vyama
vya siasa vilionekana "kuingilia majukumu ya tume ikiwemo kujitangazia
ushindi na kupelekea mashindikizo kwa tume."
"Nimeridhika kwamba uchaguzi huu
haukiwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za
uchaguzi," alisema.
"Hivyo, kwa uwezo nilionao
natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba
kuna haja ya kurudia uchaguzi huu."
0 comments:
Post a Comment