Celina Mathew
BAA la njaa linaloikumba nchi limemuibua Mufti wa
Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ambaye amewataka viongozi mbalimbali wa
dhehebu la Kiislamu kufanya maombi maalumu kwa ajili ya taifa.
Akizungumza Dar es Salaam kwa niaba ya Mufti, Mwenyekiti
wa Halmashauri kuu Bakwata Taifa, Sheikh Khamis Mataka alisema kumekuwa na
matamko mbalimbali yanatolewa kuhusu baa la njaa, hivyo kwa kiasi kikubwa dua
hiyo itasaidia.
“Nawataka wahusika wote kuleta maombi ya toba ili tuweze
kumwomba Mungu msamaha na aijalie nchi yetu na jirani kupata mvua za kheri
zitakazosaidia kutuepusha na ukame na madhara mengine, ikiwemo baa la njaa,”
alisema Mufti huyo.
Wakati huohuo, Mufti Zubeir amewateua Sheikh Mataka na Mkurugenzi
wa Daa’wa na Tabligh Bakwata kuwa wasemaji wa baraza hilo na kwamba uteuzi huo
umeanza jana.
Katika hatua nyingine Sheikh Mataka alisema kumekuwa na matumizi
yasiyo sahihi ya wadhifa wa Sheikh Mkuu kutumiwa na baadhi ya masheikh wa mikoa
na wilaya.
Alisema kwa mujibu wa Bakwata wadhifa wa Sheikh Mkuu
unamhusu Mufti wa Tanzania tu na kwamba chini yake ni Masheikh wa mikoa, wilaya
na si vinginevyo.
Masheikh wa mikoa, wilaya na mitaa wanakumbushwa kutumia nyadhifa
zao kama zilivyoainishwa katika Katiba ya Baraza kuu la Waislamu. Sheikh Lolila
astaafu Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila
amestaafu wadhifa huo kutokana na umri na afya yake.
Sheikh Lolila alisema kuwa licha ya kuomba kustaafu kwake
atakuwa tayari kulisaidia baraza pindi watakapohitaji msaada wake wa kimawazo.
“Nimeomba kustaafu Bakwata hivyo naomba watu waelewe kuwa
hali yangu inaendelea vizuri lakini watakapohitaji msaada wangu nipo tayari
nitakuja kuwasikiliza na ninapoweza nitawasaidia,”alisema.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa baraza hilo wamempongeza
kwa uamuzi huo na kuwataka wengine kuiga mfano wake kwa kuwa alikuwa kiongozi
wa mfano.
“Nampongeza sana Katibu Mkuu kwa kuona kuwa jambo hili ni
muhimu kwake kutokana na umri alionao na kama alivyosema kuhusu afya yake japo
angependa kulihudumia baraza lakini ameona inatosha kuwaachia vijana maana wazee
tuking’ang’ania watoto hawatasoma.”
“Tungependa uwe mfano wa kuigwa kwa kwa viongozi wa dini
ambao wamekuwa wagumu kujiengua, kujiuaulu au kustaafu kwenye nafasi zao waige
mfano wako, tumekuwa nae muda mrefu ndani ya baraza na tumefanya kazi kwa
uaminifu na uadilifu kwa wakati wote bila kujali likizo.”
Sheikh Mataka alisema kuwa Sheikh Lolila alikuwa mtu
ambaye pamoja na uzee alionao akiwa na kitu cha haraka hutembea kuanzia Bakwata
hadi Ikulu hivyo baraza linaandaa utaratibu maalum wa kumuaga ili kutahmini
kustaafu kwake.
Aidha nafasi hiyo itakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu wa
Bakwata, upande wa Utawala, Ustadhi Salim Abeid hadi itakapopata mtu.
0 comments:
Post a Comment