Washington DC, Marekani
Donald Trump |
MUDA mchache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 45 wa
Marekani, Donald Trump amewafuta kazi mabalozi wote wa nchi hiyo duniani na
wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa.
Trump amesema balozi katika nchi yoyote duniani ambaye aliteuliwa
na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama anatakiwa kuacha kazi mara moja.
Taarifa yake ya mabadiliko ilisema juzi kuwa hakuna
msamaha kwa yeyote kuongeza muda hata kwa mabalozi wenye watoto wadogo.
Kutokana na tamko hilo, zaidi ya mabalozi 80 wa Marekani walio
nchi mbalimbali duniani walifutwa kazi kuanzia Januari 20, mchana siku ambayo
Trump aliapishwa.
Ni kawaida kwa nafasi za kuteuliwa kisiasa, ambapo mabalozi
hujiuzulu unapoingia utawala mpya, hususan kinapoingia chama kingine
madarakani.
Inaelezwa kuwa hatua hiyo ya Trump inaweza kuvuruga
uhusiano muhimu na nchi kama vile Ujerumani, Uingereza na Canada. Ambapo nchi
hizo zinaweza kukaa bila mabalozi kwa miezi kadhaa kwa kuwa baada ya Trump
kuteua mabalozi wapya, watalazimika kuidhinishwa na Bunge la Congress kabla ya
kuanza kazi.
Pia, nchi
kama China, India, Japan na Saudi Arabia nazo zinatazamiwa kukumbwa na
mabadiliko hayo.
Uteuzi ambao umefanywa mpaka sasa ni wa Gavana wa South
Carolina, Nikki Hayley ambaye anakuwa balozi kwenye Umoja wa Mataifa akichukua
nafasi ya Samantha Power.
Mwanasheria wa Ufilisi, David Friedman ameteuliwa kuwa
balozi Israel na Gavana wa Iowa, Terry Branstad ameteuliwa kuwa balozi China.
Trump amekosolewa kwa kuacha nafasi nyingi wazi na hivyo
kuvuruga shughuli za kawaida za Serikali ya Marekani.
Hayo yanajiri huku maandamano yakiripotiwa kote duniani
dhidi ya kiongozi huyo. Imeripotiwa kuwa kumefanyika maandamano 637 katika
maeneo mbalimbali ya Ulaya, Asia na Afrika kumpinga.
0 comments:
Post a Comment