Waandishi Wetu
Dk Charles Msonde |
SIKU moja baada ya Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya kidato cha pili huku shule tisa kati ya 10
zilizofanya vibaya zikiwa za Mtwara, wadau wa elimu, ukiwamo Umoja wa Wabunge
wa Mkoa huo wametaja sababu 23 za anguko la shule hizo.
Wakati sababu hizo zikianikwa, taarifa
kutoka Mtwara zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa wakuu wa shule
zilizofanya vibaya wamepewa waraka wa kuwazuia kuzungumza chochote kuhusu
matokeo hayo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu
Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde, yanazitaja shule hizo kuwa ni Chingungwe,
Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michinga, Msimbati, Salama na Lukokoda.
Katibu wa wabunge wa mkoa huo ambaye pia
ni Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota alizitaja baadhi ya sababu hizo, kuwa
ni usimamizi mbovu wa sekta ya elimu ambapo alifafanua kuwa maofisa elimu
wameshindwa kufanya kazi zao ipasavyo kwa kukosa vitendea kazi.
Alitaja sababu zingine kuwa ni
kutotatuliwa kwa kero za walimu kwa muda mrefu, hali ambayo inachangia wakate
tamaa na elimu kukosa kipaumbele kama ilivyokuwa katika uuzaji wa korosho.
“Sababu nyingine ni kukosekana kwa
mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia, kukosekana kwa maabara, jamii
kukosa mwamko katika kuwekeza kwenye elimu na wazazi kutokamilisha majukumu
yao,” alisema.
Chikota alisema sababu zingine ni umbali
wa shule za mkoa huo ambapo pia hakuna hosteli, jambo ambalo linachangia
wanafunzi kukataa tamaa, wanafunzi kukosa mtu ambaye wanajifunza kwake kama
kivutio na watoto kutopenda shule.
Alisema ni jukumu la Serikali kuuangalia
mkoa huo kwa jicho la huruma, huku akisisitiza kuwa kufeli kwa wanafunzi hao
kusihusishwe na uvunaji korosho.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na
Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (Tamongsco), Benjamin Nkoya
alisema sababu nyingine ni mkoa huo kutumika kama sehemu ya adhabu kwa walimu
wanaoonekana kukosa uhusiano mzuri na wanasiasa na wanaopigia kelele uboreshaji
elimu.
Alitaja sababu zingine ni mila na
desturi, njaa, uhaba wa walimu, na walimu waliokuwa na vyeti bandia
waliofukuzwa inaweza kuwa sababu pia.
"Inawezekana mkoa huo ulikuwa na walimu
wenye vyeti bandia ambao kufukuzwa kwao kumesababisha hata kile kidogo
walichokuwa wanatoa kwa wanafunzi kukosekana," alisema.
Alisema pia Serikali imetilia mkazo
kufuatilia shule binafsi na kusahau shule zake jambo ambalo linapaswa kuachwa
kutokana na kukosa tija.
”Utakuta shule ina wanafunzi zaidi ya
200 katika darasa moja, haina maabara huku inatoa wanafunzi wa Sayansi lakini
hayo yote katika uhakiki huo hayaandikwi kama inavyofanyika katika shule
binafsi,” alisema.
Alisema sababu nyingine ni walimu
kupanga migomo kwenye shule za Serikali, kukosa vitabu na taarifa za ukaguzi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiah Oluoch alisema idadi ya walimu katika shule za Serikali ni
tofauti na shule binafsi.
"Shule nyingi za Serikali mazingira
si rafiki, kwa mfano hadi sasa shule za msingi zina uhaba wa walimu 100,000
huku wahitimu zaidi ya 30,000 hawajaajiriwa, na asilimia 75 ya shule hizo ziko
vijijini ambazo pia hukumbana na changamoto mbalimbali," alisema.
Aidha, Mtwara alisema kuwa mila na
desturi, uhaba wa walimu ndizo zimekuwa zikichangia wanafunzi kufeli, hivyo
alitumia nafasi hiyo kupongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mkoa huo na
kubainisha kuwa wamejitahidi sana.
Aliitaka Serikali kuboresha mazingira na
maslahi ya walimu ili waweze kufundisha vizuri na kuanzisha programu ya chakula
shuleni.
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine
Ndungulile alisema mfumo wa elimu na mitaala vinaweza kuwa sababu za matokeo
mabaya ya mitihani nchini.
Ndungulile alisema ni wakati wa wadau kukutana
na kujadili changamoto zinazoikumba mikoa ambayo inafanya vibaya katika
mitihani ya elimu ya msingi na sekondari nchini, ili kupata mafanikio.
“Mbaya zaidi wanafunzi wanafeli masomo
ya Sayansi na Hisabati ni hatari kwa Taifa ambalo linataka kuwa la viwanda,”
alisema.
Wakati wadau wakiwa na mitazamo hiyo
inasemekana katika Manispaa ya Mtwara, walimu wa shule wamepewa waraka kuwataka
kutozungumzia hali hiyo.
Walimu hao walisema kweli hali ni mbaya
na changamoto ni kubwa, lakini hawana ruhusa ya kuzungumzia jambo hilo kinyume
na hapo, hadi mwandishi wa habari afuate taratibu za kupata kibali kwa
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.
“Hatuna nafasi ya kulisemea hili sisi
walimu lakini kielimu hali Mtwara bado jitihada kubwa zinahitajika ili
kuisaidia, mimi naomba tu ufuate taratibu husika,” alisema kwa masharti ya
kutotajwa jina gazetini
Diwani wa Majengo, Ziha Khalidi akiwa
mzazi alisema jambo hilo si la kawaida kwa mkoa huo, ambapo alitaka kuwekwa
mazingira mazuri ya walimu yakiwamo madarasa ya kufundishia, nyumba za walimu,
kuwezeshwa kifedha na masuala mengnine ambayo yatamfanya mwalimu kuwa na moyo
wa kufundisha.
Ofisa Elimu wa Mkoa, Fatuma Kilimia
alipopigiwa simu na gazeti hili kutaka azungumzie hali hiyo alishindwa kuizungumzia.
Mkurugenzi wa Manispaa simu yake iliita
bila majibu huku Mkuu wa Mkoa, Halima Dendegu akisema yuko kwenye kikao na kuahidi
kumpigia simu mwandishi, lakini hakufanya hivyo jana.
Imeandikwa
na Suleiman Msuya, Emerciana Athanas na Sijawa Omary
0 comments:
Post a Comment