*Ashindwa kutaja faida za Dart kama alivyoagizwa
*Asema suala hilo
lina misuguano ya wadau wa mradi
Celina Mathew
Rais John Magufuli |
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutaka apelekewe
taarifa za faida ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene, ameshindwa kueleza faida za mradi huo.
Akizungumza juzi katika uzinduzi wa mradi huo wa awali,
Rais Magufuli alishangaa hotuba zote zilizotolewa katika uzinduzi huo, ikiwamo
ya Simbachawene na ya Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa, kushindwa kueleza faida ya mradi huo.
Kutokana na kasoro hiyo, Rais Magufuli aliagiza apelekewe
taarifa za faida ya mradi huo unaotoa huduma kwenye barabara ya Morogoro, kwa
kuwa umejengwa kwa mkopo wa Sh bilioni 403, ambazo zinatakiwa kulipwa na kuonya
kuwa akiletewa taarifa ya hasara, atatumbua wahusika.
Waziri
Akizungumzia agizo hilo jana, Waziri Simbachawene alitoa
taarifa za mapato tu, bila kueleza gharama za uendeshaji na kukiri kuwa hawezi
kuzungumzia faida au hasara za mradi, kwa kuwa inahitaji mjadala.
“Ni suala la kukaa chini na kujadiliana, huwezi kusema tu
hasara, ndiyo maana mimi nimejaribu kutoa mwelekeo wa makusanyo na mapato, sasa
ni ngapi, zimekuwaje, zimefanyikaje ni suaala la kimahesabu,” alisema
Simbachawene.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo ulipoanza Mei mwaka
jana makusanyo kwa mwezi yalikuwa Sh milioni 800, baadaye yakapanda hadi Sh bilioni
moja kwa mwezi, ikaendelea hadi Sh bilioni mbili na hadi Desemba, mradi ulikuwa
umeingiza zaidi ya Sh bilioni 19.
Misuguano
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hawezi kuwa tayari kutoa
mahesabu, kwa kuwa biashara yenye wabia wengi, lazima iwe na misuguano ambayo
inapaswa kufanyiwa uchambuzi na kupata jibu moja.
“Unapokuwa na biashara yenye wabia wengi si jambo jepesi
la kudhani inaweza ikawa imekuwa moja jumlisha moja sawa na mbili, lazima
kuwepo misuguano, huyu anasema hivi na yule anasema vile, lakini hayo sasa
tunaweza kufanya uchambuzi na kutoka na jibu moja,” alisema.
Simbachawene alisema jambo kubwa na la msingi ni kwamba Dart
wanalipwa chao, Sh milioni 8.1 kwa siku, kwa ajili ya matumizi ya miundombinu.
“Tumeona bora ya huo mfumo kuliko kuingia kwenye mahesabu,
kwa hiyo mwanzo walikuwa wanalipwa Sh milioni 4.4 kwa siku, Bodi yangu
ikanishauri, tukafanya uchunguzi.
“Baada ya uchunguzi wakasema hapa tunaweza kufanya hiki, hivyo
kwa sasa mradi ule unailipa Dart Sh milioni 1.8 bila kukosa na inakatwa kwenye
mfumo.
“Sasa unajiuliza je, Dart na wenyewe kwa matumizi ya Sh milioni
8.1 kwa siku, ukipiga mara 30 inapata Sh milioni 200 na zaidi je, wanaweza
kujiendesha au kulipa mishahara na mambo mengine? Unaona hii inawezekana,”
alisema.
Matarajio
Alisema mradi huo unaweza kujiendeshwa vizuri na hadi
sasa una abiria 200,000 kwa siku, lakini
wakipata abiria 450,000 watapata fedha
nyingi na kurudisha gawio serikalini.
Akifafanua, Simbachawene alisema hapo alizungumzia fedha inayopelekwa
Dart tu, lakini bado asilimia 41 zilizo kwenye uendeshaji za Simon Group, kwa kuwa
Serikali pia ina asilimia 49 na Simon Group ina asilimia 51.
Kutokana na hisa hizo 49 za Serikali, Simbachawene
alisema kuna gawio na kwamba fedha za gawio pia zinaingia serikalini kupitia Wizara
ya Fedha na Mipango, ambapo ikijumilishwa na inayokwenda Dart, inakuwa si haba.
Waziri alisema hayo bila kuchanganua gharama za mradi ili
kubaini faida, wakati juzi Rais Magufuli alionya kuwa tangu alipoanza kutambua
biashara, hajawahi kuwa na tafsiri inayoonesha hasara.
Mradi huo ambao kwa mujibu wa matarajio ya Rais Magufuli,
unapaswa kuwa wa faida, ni awamu ya kwanza, kwa kuwa awamu zingine zinafuata
ili kuondoa hasara ya Sh bilioni 411.55 wanayopata wananchi kwenye foleni za
Dar es Salaam kila mwaka.
Awamu zingine zitakazojengwa miundombinu ya mabasi ya
kasi na kuanza kutoa huduma hiyo ni kutoka Gerezani, Kariakoo mpaka Mbagala Rangi
Tatu, kwa awamu ya pili.
Awamu ya tatu ni kutoka barabara ya Bibi Titi Mohamed
hadi Gongo la Mboto, huku awamu ya nne ikihusu barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda
Bagamoyo, kipande chenye urefu wa kilometa 25.
Katika awamu ya tano, miundombinu hiyo itajengwa na
huduma kuanza kutolewa kwenye kipande cha kilometa 22.8 barabara ya Mandela,
huku awamu ya sita na ya mwisho ikihusu barabara ya Mwai Kibaki yenye kipande
cha kilometa 27.6.
0 comments:
Post a Comment