Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema
wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha kwenye halmashauri
zote nchini na pia hazitakiwi kuwa pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa
wabadhirifu walioshindikana kwingineko.
Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali za
mitaa na halmashauri zote nchini zinatakiwa kujitathmini na kujipanga vizuri
zaidi kuona jinsi zitakavyokuwa chachu ya maendeleo ya viwanda tarajiwa.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati
akifungua kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani hapa. Alisema kikao ni
chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitasaidia kusukuma maendeleo ya mkoa
na kupunguza migogoro kwenye halmashauri.
Alisema Serikali itaendelea kuongeza
ruzuku kwa halmashauri zote nchini kwa kadri uwezo utakavyoruhusu na kusisitiza,
kuwa fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri na zielekezwe kwenye miradi ya
maendeleo inayogusa wananchi.
“Endapo itabainika kuwapo baadhi ya sheria
zinazokwamisha utendaji katika mamlaka za serikali za mitaa, hatutasita
kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili ziendane na azma yetu ya kutoa
huduma bora kwa wananchi,” alisema.
Alisema Serikali Kuu ina maslahi makubwa
kwa serikali za mitaa, si tu kwa kuwa ni Serikali kamili katika ngazi hiyo,
bali pia kutokana na ukweli kwamba kero nyingi za wananchi ziko ngazi hiyo.
Waziri Mkuu alisema vyanzo vingi vya
mapato ya Serikali vinapatikana kwenye halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni
kulegalega kwa halmashauri nyingi katika ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya
kodi, jambo linalozorotesha utoaji huduma kwa wananchi.
Hivyo Waziri Mkuu alitoa rai kwa halmashauri
hizo kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na
kwa wakati pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza kasi ya
ukusanyaji mapato.
Pia alizitaka zihakikishe malipo yote
yanafanyika kielektoniki na zihamasishe vijana na kina mama wajiunge na vikundi
vya uzalishajimali na kuwapa stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili
kuwa chanzo cha mapato baadaye.
Alisema watendaji wa halmashauri
wanatakiwa kujiepusha na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma na uzembe kazini
na watakaobainika kufanya vitendo hivyo
wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.
“Someni taarifa ya CAG (Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na kutoa majibu ya kina ya namna
mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na ubadhirifu kama ilivyoainishwa kwenye
ripoti hizo,” alisema.
Hata hivyo, alitaka kila Halmashauri
iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo makubwa ya
kipaumbele, kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule, maboresho kwenye sekta ya
afya (ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo vya afya).
“Endeleeni kuwa na uhusiano mzuri
miongoni mwenu, fanyeni kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize
wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro, matusi,
dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane, na jamii ione mko wamoja,” alisema.
0 comments:
Post a Comment