Mwandishi Wetu
RAIS John Magufuli amesema taarifa zinazoenezwa kuhusu
nchi kukumbwa na njaa si za kweli na kuwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii
ili kujipatia chakula.
Akihutubia wananchi wa Bariadi jana alikokwenda
kuwashukuru na kuzindua ujenzi wa barabara na hospitali ya mkoa wa Simiyu, Rais
alituhumu baadhi ya wafanyabiashara walioingiza mahindi nchini na kutafuta njia
ya kuyauza.
“Kuna wanasiasa na baadhi ya waandishi wa habari
wanaotumika na wafanyabiashara walioingiza mahindi kwa njia zao na sasa
wanatumia kisingizio cha njaa ili kuuza mahindi hayo,” alisema Rais.
Alisisitiza kulima mazao yanayostahimili ukame na wenye
uwezo wa kumwagilia wafanye hivyo ili kuondokana na njaa kama itatokea mvua zisinyeshe.
“Inashangaza mtu kulima mahindi ambayo yanahitaji maji
mengi na kuacha kulima mtama ambao hauhitaji maji mengi, mtu analima mahindi kandoni
mwa ziwa, lakini anashindwa hata kuchukua ndoo kuchota maji na kumwagilia,”
alisema Rais.
Akisisitiza taarifa za madai ya njaa, rais alitolea mfano
wa ng’ombe 17,000 kufa kwa njaa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, akisema hiyo
ni taarifa ya kutunga.
“Haiwezekani unaona ng’ombe mmoja anakufa, wa pili, 100…
ng’ombe elfu…wanakufa unaangalia tu kwa nini usiwauze ukanunua chakula,
ukanunua mahindi? Hii haiingii akilini,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza
kutokuwapo njaa nchini.
Hata hivyo, alirudia kauli yake kwamba serikali haina
shamba hivyo watakaokumbwa na njaa kutokana na kutolima, wasitarajie Serikali
iwapelekee chakula na badala yake wafanye kazi ya kujizalishia chakula.
“Hata Baba Askofu yuko hapa, anajua kwamba maandiko
yanasema asiyefanya kazi na asile … usipofanya kazi ukakosa chakula basi ufe
tu,” alisema Rais na kuwataka watanzania kujiandaa kusikia na kuukubali ukweli.
“Kama mlizoea kusikia mazuri tu na sasa mjiandae pia
kusikia mabaya, mimi nitasema ukweli daima, siwezi kuita jiwe mchanga
uliojikusanya,” alisema.
0 comments:
Post a Comment