Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amesema hatua
anazochukua kurekebisha nchi na kusababisha watu kulalamika hazitabadilika na msimamo
wake uko palepale.
Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa
uzinduzi wa barabara ya Bariadi- Lamadi mkoani Simiyu yenye urefu wa kilometa
71.8 ambayo itagharimu Sh bilioni 90 hadi kukamilika kwake.
Alisema cheo ni dhamana na kwamba mtu
mwenye hofu ya Mungu lazima atekeleze alichoahidi, hivyo atahakikisha
anatekeleza aliyoahidi licha ya baadhi ya watu kulalamika.
"Kwenye kila zuri lazima mabaya
yawepo, nilisimamia kwenye ufisadi, wizi na mambo mbalimbali, lakini hatua hiyo
imenifanya nichukiwe, naomba watambue kuwa mimi nazidi kusonga mbele kwa mbele
ili kuleta maendeleo," alisisitiza.
Alisema mtendaji yoyote wa Bariadi
atakayevuruga, asitarajie kuhamishiwa eneo lingine bali atambue kuwa atafia hapohapo
alipoharibu.
Alisisitiza kuwa hatengenezi nchi ili
kudhulumu mali za Watanzania wenye maisha duni na kwamba haiwezekani mtu
mwingine ale mali za mwenzake.
Alisema Bariadi inaongoza kwa kuuza
pamba, dhahabu, ina hifadhi ya Serengeti ambako watu wa Ulaya hufika kutazama
wanyama, hivyo haiwezekani pamoja na rasilimali hizo nchi iwe masikini.
Rais alisema kwa kiasi kikubwa
anapambana na wanaofanya nchi iwe masikini kwa kuwa hakuna mzee, kijana wala
mtoto anayependa umasikini na kila mtu anapenda kupata mahitaji ya msingi.
Alisema kwenye bajeti ya Sh trilioni
29.5 asilimia 40 yake ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu na haijawahi
kutokea kiasi kikubwa hivyo cha fedha kupangwa kwani awali ilikuwa ni asilimia
26 tu.
“Kutokana na hilo kuna watu wamelalamika
na wanazidi kulalamika na mnaosikia wanalalamika ndio walikuwa wanafaidi fedha
hizo na walalamike sana, maana nataka ziende kwenye maendeleo ya Watanzania,"
alisema.
Alifafanua kuwa hadi sasa amenunua ndege
sita na hakuna nchi iliyoweza kuleta watalii bila ndege zake, hivyo ameamua
kuinua utalii ili ifikapo mwakani Bariadi iwe na uwanja mkubwa wa ndege.
Alisema kupitia fursa hizo, uchumi wa
wana Bariadi utaimarika na wafanyabiashara watafanya biashara zao vizuri na kujipatia
kipato.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga
kuhakikisha miradi ya barabara inaendelea na alimwagiza Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ahakikishe eneo la kiliometa
51.3 lililobaki la barabara linajengwa haraka na la kilometa 48.9 litangaziwe zabuni
ili nalo likamilike.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo pia utasaidia
magari yanayotoka Nairobi yaliyokuwa yanazunguka, kupita bila changamoto na
kufika kirahisi huku akiasa madereva kuwa makini barabarani ili kuepuka ajali
zisizotarajiwa.
Aliwataka wananchi wa Simiyu wasing’oe
nati za madaraja, alama za barabarani, wasimwage mafuta kwenye barabara hizo
ili zidumu kwa muda mrefu.
Akitoa maelezo ya awali, Profesa Mbarawa
alisema kati ya Sh bilioni 90 zilizotumika kwenye ujenzi huo, Sh bilioni 80 ni za
ujenzi, na zingine ni gharama mbalimbali zikiwamo za usimamizi, usanifu na
fidia kwa wananchi waliobomolewa nyumba.
0 comments:
Post a Comment