Mwandishi Wetu
Jaji Mutungi (kulia) |
SIKU chache baada ya Msajili wa Vyama
vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kuidhinisha ruzuku ya CUF kwa Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mikakati ya kumchafua imeanza chini kwa chini.
Mikakati hiyio inadaiwa kuratibiwa na
Kamati ya Uongozi ya Chama hicho ambayo Msajili haitambui.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinadai
kwamba mbinu hizo zimeanza kutekelezwa na viongozi wa Kamati hiyo kwa kusambaza
habari zinazomdhalilisha Msajili wa katika vyombo mbalimbali vya habari na
mitandao ya kijamii.
Moja ya mikakati hiyo ni iliyosambazwa
na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Mbarala Maharagande iliyojaa kejeli,
matusi, tuhuma na dhihaka kwa Msajili na kuacha kujibu hoja za msingi ambazo
awali zilitolewa na Ofisi ya Msajili.
Taarifa za ndani ya mkakati huo zinadai
kuwa pamoja na mitandao ya kijamii, pia magazeti kadhaa likiwamo maarufu la
kila wiki linalomilikiwa na wabunge wawili wa chama cha upinzani nchini
yatatumika kufanikisha azma hiyo.
Maharagande alizungumza na waandishi wa
habari huku akidai kuwa Ofisi ya Msajili inasababisha mpasuko ndani ya chama
hicho na ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Lipumba.
Aidha, JAMBOLEO ilizungumza na
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyesema Mutungi
amevunja maadili ya kazi yake, hivyo hawawezi kumvumilia.
Alisema kwa sasa wanasheria wao wako kwenye
mchakato wa kufungua kesi ili kushitaki wahusika wa wizi huo.
Akizungumzia taarifa hizo katika moja ya
magazeti, Jaji Mutungi alisema haogopi kuchafuliwa vyovyote kwa kuzingatia
ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake kwa mujibu wa
sheria za nchi na hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli dhidi yake na ofisi
yake.
"Na mimi nimezipata hizo taarifa,
kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa kunichafua, japo
naendelea kuzifanyia kazi, lakini kwa kifupi niwaambie waache wanichafue na
wala siogopi lolote," alisema.
"Mimi ni mtumishi wa umma nafanya
kazi kwa mujibu wa sharia, hivyo siwezi kuyumbishwa na mambo ya kitoto ya
kuchafuana na kurushiana tuhuma zisizo na kichwa wala miguu. Sidhani kama
kumshambulia Mutungi kunaweza kuleta tija ya wao kufikia malengo yao,"
alisema.
Aidha, alisema mjadala wa ruzuku ya CUF
aliyoitoa kwa chama hicho ameshaufunga na anashangazwa na maneno ya uongo
yanayozidi kusambazwa na watu wanaojiita viongozi wa CUF.
Jaji Mutungi alisema yeye ni muumini wa haki
na sheria, na ndiyo maana mamlaka za uteuzi zilimwamini na kumpa ujaji.
"Natambua uadilifu wangu na sitaki
niuelezee, ila nahisi tukiendelea kulizungumzia hili tutakuwa tunalikuza bila
sababu za msingi. Nasisitiza tena kuwa
ofisi yangu inamtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif Sharif
Hamad kama Katibu Mkuu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema
kinachoendelea kufanywa na kundi la watu wanaojiita viongozi wa CUF ni kuzungumza
mambo mengi ya uongo na kumhusisha bila ukweli huku wakishindwa kusoma vyema
Katiba yao wenyewe.
"Nasisitiza tena si Mutungi au
Ofisi ya Msajili iliyoandika Katiba ya CUF, ni wao wenyewe. Ofisi ilichofanya
ni kuitafsiri na kutoa mwongozo. Sasa tatizo liko wapi?” Alihoji.
0 comments:
Post a Comment