Claudia Kayombo
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo |
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ametaka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa
amani na utulivu.
Alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam kwa waumini wa Kanisa
hilo, waliofurika katika ibada ya kumbukumbu ya Wafia Dini katika Kituo cha
Hija Pugu.
“Tunapofanya ibada hii tulioombee Taifa letu, ili tuendelee
kuishi kwa amani na utulivu,” alisisitiza Kadinali Pengo.
Alisema amefurahi kushiriki ibada hiyo katika eneo hilo
la kwanza kuhubiriwa imani Katoliki katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka
1888 walipoingia Wamisionari kutoka Ujerumani.
Mahali hapo ndipo wafikia wafia dini watatu; Mtawa Martha
na mabruda Petrus na Benedikti waliouawa na wafuasi wa Bushiri aliyekuwa
kiongozi wa Wakoloni Waarabu Afrika Mashariki wakati huo.
Kadinali Pengo alisema eneo hilo ni takatifu kwa sababu
ndilo chimbuko la Kanisa hilo nchini, ambapo Wafia Dini hao kutoka Ujerumani wa
Shirika la Mtakatifu Otilien, walifika kwa moyo mkunjufu kuhubiri Ukristo.
“Nawashukuru kila mmoja wenu aliyefika hapa Pugu
kushiriki ibada hii. Tulianza ibada yetu kama mbegu ndogo ya haladali lakini
sasa tupo wengi, Mungu ndiye aliyetukusanya,” alibainisha.
Aliwataka waamini wa Kanisa hilo, kujitoa katika mambo
mbalimbali wakiiga yaliyofanywa na Wamisionari hao waliojitoa kueneza dini hiyo
bila kujali changamoto walizokuwa wakikutana nazo.
Wakati huo huo, Kadinali Pengo aliwaomba msamaha waamini
wa Parokia tarajiwa ya Msewe kwa kuwa hakuitaja miongoni mwa nyingine
alizozitaja Januari 6.
Alisisitiza kuwa hakufanya hivyo kwa makusudi na aliitaja
Parokia nyingine tarajiwa ya Baruti.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu hilo, Eusebius Nzigilwa
aliyeongoza ibada hiyo, alisema wakati Kanisa hilo likifanya kumbukumbu hizo, Taifa
lilifanya sherehe ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo aliwaomba waamini waitumie fursa
hiyo kuliombea Taifa amani na upendo.
Alisema wafia dini hao waliitika sauti ya Mungu, hivyo
Watanzania wawe tayari kujitoa kutekeleza majukumu ya jamii bila kulazimishwa.
Abate Platidius Mtunguja wa Abasia ya Ndanda alisema
Wamisionari hao wa Ujerumani walifika eneo hilo kwanza kabla ya Mt. Joseph
mwaka huo.
Alibainisha kuwa wakiwa hapo walisimika mahema waliyotumia
kusali na kuishi, mazingira ambayo yalikuwa magumu kwao, lakini walivumilia.
Alibainisha kuwa Januari 13, 1889, siku ya sherehe ya
toleo la Bwana, Wamisionari hao watatu waliuawa na yatima saba waliokuwa
wakiwalea.
Alisema kulingana na ushuhuda uliotolewa na miongoni mwa Wamisionari
waliofanikiwa kutoroka, ulikuwa wakati ambao walikuwa wakisali.
Alifafanua, kuwa Bruda Petrus ndiye alikuwa wa kwanza
kuuawa kwa kupigwa risasi kisha Bruda Benedikti aliyeuawa karibu na Tabernakulo
wakati akijaribu kumeza Ekaristi Takatifu, wakati Mtawa Martha aliuawa na mtoto
aliyekombolewa utumwani.
0 comments:
Post a Comment