Fidelis Butahe
Tundu Lissu |
WAKATI Mbunge wa Kilombelo, Peter
Lijualikali (Chadema), akiwa na siku mbili jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha
miezi sita juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu ameeleza kuwa hukumu
hiyo inatokana na vita vya kisiasa kati ya Chadema na CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye
ofisi za makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam, Lissu alisema Mbunge huyo
alianza kusakamwa siku nyingi, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi, ikiwamo ya
kupinga ushindi wake wa ubunge.
Alisema licha ya ‘vita’ hivyo, timu ya
wanasheria wa Chadema imeanza mchakato wa kuandaa notisi ya rufaa na maombi ya
dhamana ya dharura wakati uamuzi juu ya rufaa yake ukisubiriwa, kwamba taratibu
zote zitakamilika Jumatatu.
“Lijualikali na Lema (Godbless-Arusha
Mjini) ambaye yuko rumande kutokana na kunyimwa dhamana akituhumiwa kutoa lugha
ya uchochezi, wote hawa ni wafungwa wa kisiasa,” alisema Lissu.
Juzi, Mahakama ya Wilaya ya Kilombero
alimhukumu Lijualikali kifungo cha miezi sita jela kwa kufanya vurugu na
kusababisha taharuki kwenye mkutano wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Mji mdogo wa Ifakara.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Timothy
Lyon alisema kutokana na Lijualikali kuwa na kesi tatu siku za nyuma na kutiwa hatiani,
Mahakama iliona ana hatia ya kutumikia kifungo hicho huku ikimhukumu kifungo
cha nje mtuhumiwa wa pili, Stephano Mgata ambaye ni dereva wa Mbunge huyo.
Katika ufafanuzi wake jana, Lissu ambaye
pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alidai kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya Mbunge
huyo ilikuwa ya kisiasa, ili kutekeleza malengo ya CCM dhidi ya Chadema.
“Adhabu ya kifungo bila faini imetolewa
kwa sababu za kisiasa. Kwanza walimshitaki mara mbili; wakati wa kampeni za
Uchaguzi Mkuu ili wamfunge na asiweze kuendelea na kampeni. Haikuwezekana
kumfunga na alishinda ubunge,” alisema.
“Baadaye walimfungulia kesi ya uchaguzi
Mahakama Kuu ambako nako tuliwashinda vibaya. Wamekata rufaa Mahakama ya Rufani
ya Tanzania nako tutawashinda na wanajua hivyo,” aliongeza.
Alisema waliamua kumfunga Mbunge huyo bila
faini wakiamini kuwa uamuzi huo utamfanya akose sifa za kuwa Mbunge.
Huku akinukuu Ibara ya 67 (2) (c) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lissu alisema adhabu hiyo haina athari
yoyote, kwa maelezo kuwa mtu anakosa sifa za kuwa Mbunge iwapo atafungwa
gerezani zaidi ya miezi sita.
“Si kifungo tu cha miezi sita, pia
lazima awe amekutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana
na utovu wa uaminifu,” alisema.
“Adhabu ya kifungo aliyopewa Lijualikali
haijazidi miezi sita. Pia kosa la kumpiga askari Polisi, hata kama lingekuwa la
kweli, si la utovu wa uaminifu.”
0 comments:
Post a Comment