Celina Mathew
George Simbachawene |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) George Simbachawene ametoa siku tatu kwa
Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Ilala, kuhakikisha wanawaondoa wamachinga wanaofanya
biashara eneo la Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (UDART), na wasipotekeleza hilo
kibarua chao kitaota nyasi.
Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya
Rais John Magufuli kutangaza kuwa hataki kuona mmachinga yeyote anafanya
biashara kwenye miundombinu ya mradi huo na atakayekiuka atachukuliwa hatua za
kisheria.
Simbachawene aliitoa kauli hiyo Dar es Salaam
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari akisema hana nia mbaya na kauli ya
Rais kuwa wamachinga wasibugudhiwe na wasiofuata sheria lazima wachukuliwe
hatua kutokana na kusababisha changamoto kwa wapita njia na mabasi hayo.
“Rais aliposema wamachinga wasibughudhiwe
si hao wanaovunja sharia, kwa kuwa wamachinga ni wastaarabu, hawezi kuwa mtu
anayekaa kwenye barabara bali hao ni waleta fujo, aliomaanisha Rais ni wanaotii
sheria na wakiambiwa eneo hili haliruhisiwi wanaondoka angalau hata kama
halijapangwa rasmi, hupati changamoto,” alisema.
Alisema barabara hizo ni nyembamba lakini
cha kushangaza wamachinga wanafanya biashara bila woga na alisisitiza kutumia
nguvu kuwaondoa wasipotii amri hiyo na kuondoka kama wanavyotakiwa.’
“Natoa siku tatu, Mkuu wa Mkoa na wa Wilaya
kuhakikisha wamachinga walio kwenye maeneo hayo wanaondoka kuanzia Fire,
Msimbazi hadi Gerezani,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni Paul
Makonda wakati Mkuu wa Wilaya ya Ilala akiwa ni Sophia Mjema.
Alisema endapo wamachinga watarudi eneo
hilo, Mkuu wa Mkoa na wa Wilaya ya Ilala watambue kuwa kazi imewashinda, hivyo watakosa
kibarua kwa kuwa Rais aliwataka kufuata sheria na si kufanya biashara
kinyemela.
“Nikiona wamerudi, basi Mkuu wa Mkoa na
Mkuu wa Wilaya kazi imewashinda maana mimi ninayetoa maagizo haya nipo chini ya
Rais na ndiye anayeniagiza kila siku nifanye nini, kwa hiyo hakusema wafanye
wanavyotaka na kwamba hawana haki bali alisema tusiwatoe bila kuwatafutia
maeneo, hivyo watoe nafasi ili tutekeleze majukumu,” alisema.
Aliwataka kutambua kuwa wakati wao
wanatimiza majukumu yao kuna haki za watu wengine hazitakiwi kuchezewa na
kuwaomba wamsikie, wamwelewe na kisha watii amri kwa kuondoka kwenye barabara
hiyo ya BRT.
“Nadhani jana mlimsikia Rais, alisema
atakayechezea barabara ya BRT kamata peleka au choma tairi, huyo ni Rais
amesema, sasa mimi niseme nini?” Alihoji Simbachawene.
Aliwataka wamachinga waondoke kwenye
miundombinu ya barabara kuanzia Kimara-Morocco, Kimara - Feri na Kimara-Gerezani
hasa Gerezani, kwa kuwa hata eneo la kukata kona ni shida hivyo hawawezi kuacha
liendelee.
0 comments:
Post a Comment