Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameuagiza
uongozi Wizara wa Elimu, Sayansi na Telnolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili
kubaini sababu za shule tisa za mwisho katika matokeo ya Kidato cha Pili kutoka
mkoani humo.
Pia, ameziagiza halmashauri nchini
kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu,
jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo juzi wakati
akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo
ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika
hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule
10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika
Mkoa wa Mtwara na moja Tanga.
Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni
Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na
Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na
Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10
zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana
zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali na kuuagiza uongozi wa wizara hizo
kwenda mkoani Mtwara, pia waziri mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo
awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za
mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, mkuu
wa mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga alisema katika matokeo
ya mtihani Kidato cha Pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili
kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha
katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa
wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi
kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.
0 comments:
Post a Comment