Mtuhumiwa atoroka polisi, afungwa miezi 6


Jemah Makamba

MAHAKAMA ya Mwanzo Kariakoo imemhukumu kwenda jela miezi sita, Dalius Kaishema (34), raia wa Rwanda kwa kosa la kutoroka akiwa chini ya ulinzi mahakamani.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Agnes Barasobian baada ya Koplo Said wa Polisi, kutoa maelezo ya jinsi Kaishema alivyotoroka na kukimbia.

Sehemu ya mahojiano katio ya Hakimu na Koplo Said kabla ya hukumu ilikuwa kama ifuatavyo:

Hakimu: Unaitwa nani na unaweza kuelezea nini kimetokea kuhusu huyu mshtakiwa?

Akari: Naitwa Koplo Said, nikiwa eneo langu la kazi mahakamani hapa Januari 23, saa 6:20 mchana niliwatoa washitakiwa kwenye mahabusu ya Mahakama na kwenda kusomewa mashitaka.

Hakimu: Baada ya kusomewa nini kiliendelea?

Akari: Washitakiwa walisomewa hapa kwako na baada ya hapo wakati nikiwa nawarudisha mahabusu, mshitakiwa huyu alikurupuka na kuruka uzio wa Mahakama na kukimbia nilipuliza filimbi na askari wenzangu walisikia na tukamkimbiza mshitakiwa na kumkamata maeneo ya Fire.

Hakimu alimhoji mshtakiwa kama kweli alikimbia na kwa nini alifanya kitendo hicho.

Alijibu: "Hakimu kwanza kabisa mimi si Mtanzania mimi kwetu ni Rwanda, nilikuja Tanzania Julai 23, 2013 na nikiwa Rwanda nilikuwa mfuasi wa chama cha upinzani cha Rwandanziza na niliingia hapa kihalali nikiwa na hati ya kusafiria.

“Sikuwahi kupata kesi yoyote na kufanya uhalifu wowote nchini, lakini Watanzania wanashindwa kunielewa, mimi naumwa ugonjwa wa OTISM na ni watu wachache huumwa ugonjwa huo, sasa muda mwingi wananitenga na hata kesi iliyonileta nimesingiziwa.

“Nilijaribu kutoroka ili nisiende mahabusu, ilikuwa bahati mbaya Hakimu naomba UNHCR (Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi) waje kunisaidia nirudi nyumbani Rwanda," alidai mshitakiwa.

Hakimu alisema mshitakiwa anatiwa hatiani kutokana na kukimbia chini ya ulinzi baada ya kusomewa mashitaka ya wizi yanayomkabili na kwa kuwa alikiri kukimbia.

Barasobian alimwomba karani kumbukumbu za nyuma za mshitakiwa za ambapo alisema hakuna kumbukumbu za nyuma hivyo apewe adhabu liwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama yake.

Mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea kabla ya kupewa adhabu ambapo aliiomba Mahakama imsamehe na kwamba hawezi kurudia kitendo hicho.

Hakimu alisema kwa kuwa mshitakiwa alijutia alichokifanya na ni mara yake ya kwanza, basi anamhukumu kifungo cha miezi sita jela.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo