Abraham Ntambara
Ali Hassan Mwinyi |
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali
Hassan Mwinyi, amewataka wananchi wasioridhishwa
na uamuzi wa kesi zao kukata rufaa katika mahakama za juu na kuachana na kudai
haki katika vyombo vingine vya serikali nje ya Mahakama.
Rais
Mwinyi alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa wiki ya
utoaji wa elimu ya mahakama kwa umma.
Alisema
kuwa wananchi wengi hawana elimu ya sheria, hivyo kushindwa kujua hatua za
kuchukua katika kudai haki baada ya mahakama kutoa hukumu ya kesi zao.
“Nakumbuka
nikiwa Rais nilikuwa nikipokea malalamiko, ushauri wangu nautoa tena leo. Kama
haukuridhishwa na uamuzi wa Mahakama, njia sahihi ni kukata rufaa katika Mahakama
ya juu,” alisema Rais Mwinyi.
Aidha
alisema kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa masuala ya sheria na
taratibu za kimahakama, wamekuwa wakipoteza haki yao kwa kwenda kuidai nje ya
chombo cha Mahakama.
Rais
Mwinyi alisema ni ajabu kuona wananchi wakienda kudai haki ya kimahakama kwa mkuu
wa mkoa ama wa wilaya, kitu ambacho siyo sahihi.
Alieleza
pia kuwa ukosefu wa elimu ya kisheria, umekuwa ukichangia tabia ya watu kujichukulia
sheria mkononi, hviyo ni vema katika wiki hii, wananchi wakapata elimu na kujua
hatima yao katika kudai haki.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa
Ibrahim Juma aliwataka
wananchi kufahamu kuwa Mahakama ni chombo ambacho kipo kwa ajili ya ustawi wao.
“Ibara ya Nane ya Katiba inasema, mwananchi
ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho na mihimili mitatu ya dola, Mahakama, Bunge, na
utawala vipo kwa ajili ya ustawi wa mwananchi,” alisema Kaimu Jaji Mkuu Juma.
Aidha alisema kuwa sheria ni nyenzo
muhimu ya kumwezesha mwanadamu kuishi katika jamii. Akawataka wananchi
kutembelea vibanda mbalimbali katika wiki hii na kujifunza umuhimu wa utawala
wa sheria.
Alisema katika mabanda hayo watapata
kujua namna sheria zinavyofanya kazi na zote zikilenga kumsaidia mwananchi.
Kaimu Jaji Mkuu alisema mwananchi ni mtu
muhimu katika sheria, hivyo sheria lazima ilenge katika kumnufaisha.
Alisema mwaka 2008 Kamisheni ya Umoja wa
Mataifa ilisisitiza kuwa sheria zote za nchi lazima zijengwe katika kumwezesha
masikini, mizani ya ubora wa sheria hupimwa kwa jishi inavyomsaidia mwananchi
kutoka katika umasikini.
0 comments:
Post a Comment