Aidan Mhando, Mwanza
SIKU moja baada ya walimu watatu wa Serikali kukamatwa
wakifundisha shule binafsi ya Musabe jijini hapa, Serikali ya Mkoa, imesema
itawachukulia hatua za kisheria ikiwamo kutudisha mishahara waliyolipwa tangu
walipoaga kwenda masomoni.
Walimu hao wanadaiwa kwa nyakati tofauti kumuaga mwajiri
kuwa wanakwenda masomoni walikamatwa juzi na Polisi, wakifundisha shule hiyo,
huku mmoja akitoroka kwa kuruka ukuta wa shule hiyo.
Jana Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha akifuatana
na polisi walifika shuleni hapo na kuhoji walimu hao, ambapo alisema alipata
taarifa kutoka kwa wasamaria wema ya kuwapo walimu walio likizo ya masomo, lakini
wanafundisha kwenye shule hiyo.
“Huu ni wizi, kwani walikuwa wanachukua mshahara wa Serikali
na hapa wanalipwa pia. Kwa kushirikiana na wakurugenzi tutawahesabia kiasi gani
cha fedha mpaka sasa wamechukua ili kuzirudisha,” alisema Tesha.
Aliongeza kuwa ni jambo la kushangaza kuona watumishi wa
umma wanashindwa kusoma alama za nyakati, kwani kila mtu alisikia uhakiki wa watumishi
hewa, lakini bado watu hawakomi na wanaendelea kukiuka sheria, hivyo lazima
sheria ichukue mkondo wake.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Shule hiyo, Daniel
Damian alisema ilikuwa vigumu kubaini kwamba walimu hao walikuwa waajiriwa wa Serikali
kwani taratibu zote za shule walizifuata ikiwamo kusaini kitabu cha mahudhurio
wakati wa kuingia na kutoka.
“Walikuja hapa wakaomba ajira. Sisi tuliwafanyia usaili
na kuwaajiri, tuliwauliza kama waliajiriwa serikalini, walikataa. Tunashukuru
Serikali mmetusaidia kwa hili, sasa tutakuwa makini,” alisema Damian.
Ofisa Elimu ya Sekondari wa Mkoa wa Mwanza, Gwasa Joseph
alisema atafuatilia suala hilo kupata ukweli na hatua za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao, kwani kitendo hicho ni uvunjaji wa sheria na wamehusika na wizi
serikalini.
“Huu ni wizi wa hali ya juu haiwezekani unaomba kwenda
masomoni halafu unakwenda kuajiriwa kwingine. Sheria inasema wazi, kwamba
mwalimu akiomba kusoma, akiwa likizo
lazima aripoti kwa mwajiri wake,” alisema Daimin.
Walimu waliokamatwa ni Lwiza Ntare (27) ambaye alikuwa
akifundisha sekondari ya Kibehe, Chato, Geita; Richard Mgendi (30) akifundisha
sekondari ya Misasi, Misungwi mkoani hapa na Gilbert Makwaya (33).
Kati yao mmoja aliyetoroka alikuwa Makamu Mkuu wa Shule
hiyo kwa upande wa wanawake.
0 comments:
Post a Comment