Hussein Ndubikile
George Simbachawene |
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, amesema Serikali inasubiri
taarifa za uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam juu ya fedha za mauzo
ya Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA) ndipo iamue.
Hatua hiyo imekuja baada ya Rais John
Magufuli kutoa agizo la siku tano kwa Jiji hilo kuzipangia matumizi Sh bilioni
5.8 zilizopatikana baada ya shirika hilo kuuzwa na ikishindwa litoe taarifa kwa
Serikali izipangie kwa kuzipeleka.
Hata hivyo, siku tano zimemalizika na
hakuna kiongozi wa Jiji aliyetoa taarifa za wapi fedha hizo zitaelekezwa na sababu
zipi zinakwamisha utekelezaji wa agizo hilo.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu
jana, Waziri alisema baada ya siku hizo kwisha wanasubiri taarifa rasmi kutoka
Jiji kwa lilichoamua ndipo Serikali iamue wapi fedha hizo zielekezwe.
“Nasubiri kupata taarifa rasmi kutoka Jiji
la Dar es Salaam juu ya walichoamua, ili Serikali ichukue uamuzi,” alisema.
Uongozi wa Jiji uliopita uliuza shirika
hilo kwa kampuni ya Simon Group kwa kiasi hicho cha fedha, matokeo yake
kuliibuka mzozo mkubwa bungeni kwa madai kuwa kiwango hicho hakilingani na
thamani halisi ya mali za UDA.
Mbali na mzozo huo, kulitokea hali ya
kutoelewana na kutoleana lugha za matusi kati ya wabunge wa Dar es Salaam na
aliyekuwa Meya wa Jiji hilo, Didas Masaburi.
0 comments:
Post a Comment