Salha Mohamed
Moto Uwanja wa Ndege JNIA |
MOTO uliotokea katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), umeteketeza chumba cha mizigo ya abiria cha
uwanja huo na mizigo yote iliyokuwepo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema moto
huo ulitokea usiku wa kuamkia jana saa tano usiku katika chumba kidogo cha
kuhifadhia mizigo ya abiria cha kampuni Swissport, inayohudumia abiria.
Akizungumza mara baada ya kukagua eneo
lililoteketea akitokea Mwanza, Mbarawa alisema tayari ameunda timu ya watu 12 ya
kuchunguza chanzo cha moto huo ndani ya mwezi mmoja.
“Ukitokea moto watu watasema ni janga tu
limetokea, lakini kuna uchunguzi wa kitaalamu kwanini moto umetokea na sisi
tumeunda timu ya wataalamu wafanye uchunguzi wa kina kwa nini moto ule
ulitokea,”alisema.
Alisema timu hiyo yenye watu 12
inaongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu (TAA),
Joseph Nyahende ambayo anatarajia watatoa majibu ya uhakika.
“Tume hii watatoa majibu ya uhakika,
hawatatupa bahati mbaya imetokea maana kwenye utaalamu hakuna kitu bahati mbaya
kuna sababu ya msingi,”alisema na kuongeza kuwa anatarajia kupata taarifa ya
kitaalamu itakayoeleza chanzo cha moto huo.
Kutokana na ajali hiyo, alisema Serikali
imeweka mikakakti ya kuhakikisha viwanja vyote vya ndege hakutatokea majanga ya
moto kama uliotokea hapo.
“Kazi tunayosubiri ya msingi ni kupata
majibu ya wataalamu ili tuone tatizo lilikuwa nini na turekebishe matatizo yote
na si hapa tu, bali viwanja vya ndege vyote Tanzania,”alisema.
Mbarawa alisema ni lazima Serikali ihakikishe
kuwa majanga ya moto hayatokei kama lililotokea juzi.
Mbarawa aliongeza kuwa si sahihi
kumnyooshea kidole mtu kutokana na moto huo kwa sasa, kwani si sahihi hivyo
wasubiri taarifa ya wataalamu ili kuona kosa lilipo.
Aliongeza kuwa hadi sasa hawajui thamani
halisi ya mizigo iliyoungua na nini kilikuwepo ndani ya mizigo hiyo kwani
hawana mamlaka ya kuangalia kama abiria hayupo.
Katika hatua nyingine, mbarawa ametoa
miezi miwili kwa kampuni ya kusafirisha mizigo ya Swissport kurekebisha utoaji
huduma kwa abiria kwakuwa huduma zao haziridhishi.
“Swissport imekuwa ikifanya kazi peke
yake kwa muda mrefu sana hapa uwanja wa ndege, hatuwezi kujua kama huduma zao
ni mbaya lakini kwa taarifa nilizopata huduma haikidhi mahitaji,”alisema.
Alisema mwaka jana waliingiza kampuni
nyingine ya Nas Dar Airco kufanya kazi, lakini haijafanya kazi huku ikidaiwa
Swissport kuweka mazingira ya kampuni hiyo mpya kutofanya kazi.
Alisema tayari wameleta wataalamu wa
kuangalia kama kampuni hiyo inafanya ujanja ujanja kinyume na taratibu za
sheria yake.
“Kama anafanya ujanja ujanja wowote
kinyume na leseni aliyopewa, lazima tutaifuta leseni, lazima ufanye kazi na
kila mtu katika uwanja wa ndege huu umpe haki sawa…kama mlizoea hivyo wakati
huu sio.
“Wakati umepita lazima mfanye kwa
utaratibu na kanuni zilizowekwa, vinginevyo kama hamkufanya hivyo nikiletewa
leseni mimi naifuta,”alisema.
Alisema anaamini ufanisi utakuwepo kama
kutakuwa na kampuni nyingi zinazofanya kazi katika uwanja huo kwa kuwa baadhi
ya mashirika ya ndege yameanza kulaumu huduma za Swissport.
“Nasema si kwa sababu ya moto lakini
nasema kwa sababu awali huduma zako hazipo vizuri, watu wamelalamika sana
tumekupa fursa tumia fursa vizuri tuwaletee wasafiri wetu huduma
nzuri,”alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Swissport,
Mrisho Yasin alisema tuhuma hizo ndiyo amezisikia kwa Waziri, hivyo
watazifanyia kazi na kutoa mrejesho.
0 comments:
Post a Comment