Salha Mohamed
WANAWAKE wanamiliki asilimia tisa tu ya
ardhi au mashamba nchini, ingawa kundi hilo ndilo linalozalisha chakula kwa
asilimia 60, ikilinganishwa na wanaume.
Hayo yalibainisha Dar es Salaam jana wakati
wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu Mradi wa Uhamasishaji wa Usawa wa
Kijinsia katika Kilimo, uhakika wa Chakula na Lishe kutoka Shirika la Land
O’Lakes.
Mshauri Mwelekezi wa Usawa wa
Kijinsia wa shirika hilo, Magreth
Henjewele alisema tafiti zinaonesha kuwa kilimo ni nguzo ya taifa kwa kuwa
maendeleo ya uchumi yanakitegemea.
“Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka
jana inaonesha kilimo ndiyo kinaongoza kwa kuchangia asilimia 29 katika pato la
taifa ukilinganisha na sekta nyingine,”alisema.
Alisema wanawake ndiyo wenye mchango
mkubwa katika kilimo, lakini humiliki ardhi kwa asilimia ndogo ambapo katika
utafiti wa masuala ya kazi wa mwaka 2014 unaonesha wanawake huchagia zaidi ya
asilimia 51 ya nguvu kazi katika kilimo.
Magreth alisema katika uzalishaji mazao
ya kilimo wanawake wamekuwa wakishiriki zaidi, huku wakiwa hawanufaiki na kile
walichokizalisha.
Alisema jamii inatakiwa kuelimika katika
masuala ya kijinsia katika kilimo na mgao wa manufaa kutokana na uzalishaji wa
mazoa ya kilimo.
Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dk Rose
Kingamkono alisema mbali na kilimo kuwa uti wa mgono lakini kinatoa ajira
takribani asilimia 70 hapa nchini.
“Bahati mbaya sekta ya kilimo imegubikwa
na nyenzo ambazo ni duni, na kusababisha uzalishaji wake kutokuwa mzuri huku nguvu
kazi kubwa wakiwa ni wanawake,”alisema.
Alisema kutokana na nyenzo duni wamekuwa
wakitumia muda mwingi katika uzalishaji na kuathiri afya zao pamoja na watoto
waliopo tumboni kwa wajawazito.
Alisema hadi sasa tayari wametoa semina
25 katika kaya 7000 katika mikoa wa Morogoro, Iringa, Dodoma kwa wananchi ili
kujua usawa wa kijinsia katika kilimo kama upatikanaji wa ardhi, kufanya kilimo
biashara na hata kujua sheria zilivyo.
Aidha mtafiti na mchambuzi wa sera na
masuala ya kijinsia, Profesa Bertha Koku alisema amegundua kuwa katika sera za
hapa nchini zinamaeneo ya uwezeshaji na kumsaidia mwanamke kujikomboa na
kujiimarisha katika uchumi, kimaisha, kisiasaa kupata haki zake na rasilimali.
“Katika sera hizo tumegundua kuwa kuna
maeneo ambayo ni kandamizi hivyo tunaendeleza pale ambapo tunaona mwanamke
anaweza kunufaika na kilimo na kunufaika na jasho lake,”alisema.
Alisema juhudi zichukuliwe na taasisi
zingine katika kuhakikisha wananchi wanaelewa hasa katika kujiendeleza katika
kilimo kwa wanawake na hata kusaidiana kazi ngazi ya familia.
Alisema kuna umuhimu wa kutangaza sera
na watu wazifahamu ili wazitumie katika kudai haki zao kwani hawazifahamu na
kushindwa kuzitekeleza.
“Sera kwa kiasi kikubwa ni nzuri lakini
utekelezaji ndiyo unakuwa na matatizo sana basi tujaribu kuona mikakati gani
inatumika ili watu wazifahamu na kuzitekeleza,”alisema.
0 comments:
Post a Comment