Suleiman Msuya
WAJAWAZITO wameshauriwa kuanza kliniki
miezi mitatu baada ya kugundua kuwa wana mimba ili kuepusha magonjwa ambayo
yanawakumba katika kipindi hicho.
Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa
Kigamboni, Dk Faustine Ndungulile ambaye kitaaluma ni daktari wa kutibu
binadamu wakati akizungumza na JAMBOLEO jana ambalo lilitaka kujua sababu zinazosababisha
vifo vya wajawazito nchini.
Alisema pamoja na utafiti kuonesha kuwa
asilimia 51 ya kina wajawazito ndio wanahudhuria kliniki bado kuna changamoto
ya walio wengi kujifungulia majumbani.
Mbunge huyo alisema kitaalamu mjamzito
anapaswa kuanza kliniki miezi mitatu baada ya kujigundua kuwa mjamzito.
Alisema iwapo wajawazito watazingatia
taratibu za kiafya ni dhahiri madhara yanatokana na mimba yatakuwa yanapungua
siku hadi siku.
Dk Ndugulile alisema utafiti unaonesha
kuwa kati ya wanawake 100,000 ambao wanajifungua, 555 wanapoteza maisha nchini
idadi ambayo ni kubwa na kuwa sababu ya vifo hivyo ikiwa ni kifafa cha mimba, shinikizo
la damu, kutokwa na damu na maradhi tofauti.
Alisema asilimia 63 ya wajawazito ndio
wameonekana kujifungulia hospitalini hiyo ikionesha kuwa asilimia 37
wanajifungulia katika mazingira yasiyo sahihi.
“Unajua mwanamke kupata mimba ni sifa ya
ukamilifu wa afya yake na tambua kuwa mimba si ugonjwa hivyo kuumwa mjamzito si
kipaumbele katika mimba,” alisema.
Alisema kinachohitajika ni wajawazito
kufuata taratibu za uzazi kwa umakini ikiwa ni pamoja na kula vyakula ambavyo
vina kinga mbalimbali.
Mbunge huyo alisema wajawazito wanapaswa
kujiepusha na msongo wa mawazo, presha ambazo huwa zina matokeo ya kusababisha
kifafa cha mimba.
Aidha, alisema hata changamoto za
kimaisha zinasababisha magonjwa yasiyotarajiwa kwa wajawazito.
Akizungumzia wilaya ya Kigamboni,
alisema kitakwimu hali ni nzuri tofauti na vijijini na kuwa sababu kubwa ni
kuwepo vituo vya afya ambavyo vina kila huduma yakiwamo magari ya kubebea
wagonjwa.
0 comments:
Post a Comment