Abraham Ntambara
Jaji Mutungi |
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
imesisitiza msimamo wake kwamba Chama
cha Wananchi (CUF) ni kimoja, hivyo yeyote mwenye malalamiko ayapeleke ofisini
ili yashughulikiwe na si kulalamika kupitia vyombo vya habari.
Kauli hiyo imekuja baada ya mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius
Mtatiro kueleza jinsi Profesa Ibrahim Lipumba alivyochukua fedha za ruzuku
zaidi ya shilingi milioni 369 kutoka Hazina.
Mtatiro anamtaja msajili, Jaji Francis
Mutungi kuwa anafahamu na kuidhinisha mchakato huo wakati Oktoba 10 mwaka jana,
aliandika barua ya kusitisha utoaji wa ruzuku kwa chama hicho kutokana na
mgogoro hadi hali itakapokuwa shwari kiutendaji.
Lakini mwishoni mwa juma, mkuu wa
Kitengo Cha Mawasiliano katika ofisi hiyo ya Msajili, Monica Laurent alieleza
kuwa kuna chama kimoja tu cha CUF.
“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
inatambua CUF iko moja tu, Kama CUF kuna watu wana malalamiko ya msingi wayalete
rasmi ofisini, huo ndiyo msimamo wetu,” alisema Laurent.
Aidha aliwataka kutumia mfumo rasmi wa kuwasilisha
malalamiko hayo kwenye ofisi ya msajili, akibainisha kuwa ofisi hiyo haiwezi kujibu
masuala hayo kwenye vyombo vya habari.
Hivi karibuni Mtatiro akizungumza na
vyombo vya habari alieleza kuwa tangu Msajili aandike barua ya kusitisha ruzuku,
chama kinadai Hazina sh. 635 Milioni, hivyo CUF haitambui utaratibu mwingine uliotumika kuigawa ruzuku
hiyo hadi Lipumba akapata mgawo wake.
Alisema chama kimeibiwa fedha za ruzuku
sh. 369 ambazo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Kuu Januari 5 na
kuingizwa kwenye akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The Civic United
Front, ikiwa ni akaunti namba 2072300456.
0 comments:
Post a Comment