Moses Ng’wat, Mbeya
MWENYEKITI wa CCM wa Wilaya ya Mbeya,
Ephaim Mwaitenda, amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Mwaitenda ambaye kwa sasa amelazwa
katika hospitali ya Rufaa Mbeya akiendelea na matibabu, alipigwa risasi mgongoni
akiwa amelala usiku wa manane wa kuamkia jana kibandani shambani mwake, Kyela.
Akithibitisha tukio hilo jana, Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Emmanuel Lukula alisema tukio hilo lilitokea juzi
saa nane usiku shambani kwake.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda Lukula alisema
hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa ingawa taarifa za awali zinaonesha kuwa
huenda tukio hilo lilifanywa na watu wa karibu na Mwenyekiti huyo.
Akifafanua alisema kabla ya watu hao
kumjeruhi Mwenyekiti kwa risasi walitoboa dirisha kwa kukata nyavu na kuingiza
mtutu na kumfyatulia risasi mgongoni.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa
bunduki iliyotumika kwenye shambulio hilo ni ya kienyeji kwani risasi
zilizotumika ni golori na kama ingekuwa ni bunduki ya kisasa asingenusurika,”
alifafanua Kamanda Lukula.
Hata hivyo, Kamanda alisema baada ya
watu hao kutekeleza tukio hilo, walikimbilia kusikojulikana bila kuchukua kitu
chochote.
“Jitihada za kuwakamata waliohusika zinaendelea
kwa kuwa askari Polisi waliofika eneo la tukio walipata baadhi ya vitu muhimu
katika uchunguzi vinavyodhaniwa kudondoshwa na watu waliotekeleza tukio hilo,”
alisema Kamanda.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Zongo
Lobe Zongo alisema hali ya Mwenyekiti huyo inaendelea vizuri kutokana na
jitihada za madaktari wa Hospitali ya Mbeya kumfanyia uchunguzi wa awali, ikiwamo
kumtoa risasi mwilini.
“Kama utakuwa mvumilivu naomba unipigie
baada ya muda kwani hivi sasa tuko hapa X-ray (Chumba cha Mionzi) madaktari
wanampiga picha ili wakamtoe risasi, lakini hali yake si mbaya, kwani nimeongea
naye,” alisema.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya
Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji akizungumzia hali ya majeruhi baada ya
kupokewa hospitalini hapo, alisema hali yake inaendelea vizuri na alipelekwa
chumba cha upasuaji kutolewa risasi.
“Alikuja hapa akiwa na hali nzuri kwani
anazungumza na tulipomfanyia vipimo vya awali kama presha ilikuwa sawa na baadaye
mchakato wa kumfanyia uchunguzi wa jeraha lake mgongoni ambalo linaonekana kama
limetobolewa na bisibisi na kwa mtazamo ni risasi za mtawanyiko,” alifafanua Dk
Mbwanji.
0 comments:
Post a Comment