Salha Mohamed
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na
Michezo, Nape Nnauye amelitaka Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) kubeba
ajenda za Serikali ya Viwanda.
Aidha, Rais John Magufuli ameahidi
kutembelea ofisi za magazeti hayo kwa kushitukiza ili kuona utendaji kazi wao.
Nape alisema hayo Dar es Salaam jana kwenye
maadhimisho ya miaka 10 ya gazeti la Habari Leo.
Alisema shauku yake ni kuona gazeti hilo
likibeba ajenda za Serikali Viwanda.
“Ningetamani mbebe ajenda za Serikali
kama Serikali ya Viwanda, kwa kuhusisha wananchi moja kwa moja,” alisema Nape.
Alisema asilimia 80 ya wananchi ni
wakulima, hivyo wanapaswa kuwaaminisha kuwa fursa ya viwanda ni yao na si ya Serikali.
Aliongeza kuwa kupitia gazeti lao,
wanatakiwa kudumisha utamaduni na sanaa kwani tayari kuna utamaduni ambao unaanza
kupotea.
“Mjali haki za watumishi, muwe wasikivu
kwa mambo yao, msiyapuuze muwasikilize na kuwatendea haki…mkiwajali hawa
mtapata baraka za Mungu,” alisema.
Aidha, Nape aliwataka kuwa wabunifu na
kuongeza motisha kwa wafanyakazi.
Awali, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim
Yonazi alisema mbali na mafanikio waliyopata katika miaka kumi ya gazeti hilo
wamejizatiti kutoa yale jamii inayoyataka.
“Kuelekea miaka kumi ijayo, gazeti letu
litabadilika kuwa kampuni ya ushauri na kutengeneza fedha nyingi na si tu
kuchapisha magazeti,” alisema.
Gazeti la Habari Leo lilisaini
makubaliano ya kukuza Lugha ya Kiswahili na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita)
na kuzindua bahati nasibu ya watoto waliozaliwa au kutimiza miaka kumi Desemba
21.
0 comments:
Post a Comment