Abraham Ntambara
Hamad Yusuf Masauni |
WATU mbali mabali wamelaani kauli ya
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliyoitoa juzi akiwa Rukwa akiagiza Jeshi la Polisi kukamata
wanasiasa watakaotangaza kuwapo njaa nchini.
Hivi
karibuni, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) liliandika barua kwa maaskofu wa makanisa
yote nchini kuliombea Taifa ili mvua inyeshe kwa kuwa kipindi hiki kilikuwa kinatarajiwa
kuwa na mvua lakini hali imekuwa tofauti.
Ilifuatiwa
na taarifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) nalo likiwataka maimamu
na mashehe misikitini kuongoza Waislamu kuliombea Taifa lipate mvua na kuondoa
ukame na baa la njaa linalolinyemelea.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO jana Dar es Salaam, watu hao walisema kauli
hiyo haina mantiki, hivyo kumtaka ahimize Polisi itimize wajibu wake wa kulinda
usalama wa raia na mali zao, kwa kuwa agizo lake linakiuka Katiba inayompa mtu
uhuru wa kutoa mawazo.
Mbunge
wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema kauli ya Naibu Waziri kuzuia
watu kuzungumzia njaa na kuagiza watakaokiuka wakamatwe ni kinyume na Katiba, inazuia
uhuru wa kutoa maoni.
Kafulila
alisema kauli hiyo haina tija na Jeshi la Polisi lina shughuli nyingi za
kufanya kuliko agizo hilo, hivyo ingekuwa busara kama angelihimiza kuhakikisha
linalinda usalama wa raia.
“Hata
Rais alipokataza watu kuzungumzia njaa, TEC na Bakwata walisisitiza msimamo wa
kuwapo dalili za njaa,” alisema Kafulila.
Mkurugenzi wa
Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliilaani agizo hilo kwa maelezo kuwa ni
kauli isiyo ya kitanzania.
“Haiwezekani
watu wana njaa wakae kimya kwa sababu wanaogopa kukamatwa,” alisema Mrema.
Aidha,
alisema ilitakiwa waanze kukamata viongozi wa dini waliotangaza kuliombea mvua
Taifa, ambapo alibainisha kuwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere hatukuwahi
kuwa na viongozi wenye kauli za namna hiyo wasiotaka wananchi kusema ukweli wa
hali halisi.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alisema kauli hiyo haina maana
yoyote kwa sababu si vibaya kusema kuwa sehemu fulani kuna njaa.
“Kama
atasubiri Rais atangaze kuwapo njaa, yeye aendelee kumsubiri, Rais atatangaza
wakati yeye anakula,” Alihoji Mtatiro.
Alisema
vijijini kuna njaa na hali inazidi kuwa mbaya ambapo alieleza kuwa kama kauli
yake itakuwa hivyo, afungue magereza ya kuwaweka kwa kuwa hawataacha kusema
kuna njaa nchini.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Jamii kwa
Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga alisema
kauli hiyo imekosa weledi, kwa kuwa hakuna anayependa njaa akieleza kwamba Rais
alikwishasema hakuna njaa.
“Rais
anaposema hakuna njaa ina maana kwamba hata ikiwapo yuko tayari kushughulikia,”
alisema Askofu Mwamalanga.
Alisema
kauli hiyo ni ya kutaka kumfurahisha Rais ambapo alibainisha kuwa hiyo si kazi
yake kwa kuwa Mkuu wa Nchi alikwishasema na badala yake alitakiwa kuliagiza
Jeshi la Polisi kusimamia usalama wa raia na si vinginevyo.
Masauni
Hata
hivyo, Masauni alifafanua kuwa kauli yake ilitokana na taarifa ya mkoa wa Rukwa
kuonesha kuwa eneo hilo halina njaa, hivyo akaonya kuwa hatarajii kusikia watu
watakaojitokeza kusema kuna uhaba wa chakula mkoani humo.
Isitoshe
alisema taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ilionesha kuwa mkoa
una chakula cha ziada, lakini kuna baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwapo njaa
mkoani humo.
“Kauli
ya Mkuu wa Mkoa ni sawa na ya Rais katika eneo hilo. Sitarajii mwanasiasa au
mtu yeyote kutoa taarifa kwamba mkoa wa Rukwa unakabiliwa na njaa. Ikitokea hivyo, utakuwa ni uchochezi hivyo
mhusika kustahili kuchukuliwa hatua,” alisema Masauni.
0 comments:
Post a Comment