Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
SI jambo la kawaida kutokea kiongozi wa kuteuliwa na
Rais, akajiuzulu nafasi yake ili akafanye shughuli binafsi, isipokuwa kutokana
na kashfa zinazoiathiria jamii pana hasa katika upatikanaji wa huduma za kijamii.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel
Mnyele, ametangaza kuachana na kazi hiyo, baada ya kumuandikia barua Rais John
Magufuli, akiomba ombi lake likubaliwe akafanye shughuli binafsi.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imethibitisha
kujiuzulu kwa Mnyela na kwamba Rais John Magufuli alilikubali ombi hilo. Hivi
sasa Mnyele ambaye ni mwanasheria anarejea kwenye shughuli binafsi ambazo si
lazima umma kuzijua, kwa maana hayupo tena katika utumishi wa umma.
Pamoja na Mnyela, ninatambua kuwapo wateuliwa wengine
waliowahi kufukia hatua kama ya Mnyele, muda mfupi baada ya kuteuliwa kwao.
Miongoni mwa hao ni aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ally Masoud
Maswanya, akajiweka kando kushika wadhifa huo hata kabla ya kuapishwa.
Matukio hayo mawili na mengine yanayofanana na hayo,
yanaweza kuwa moja ya vigezo vinavyoweza kubatilisha hisia hasi juu ya hatua iliyofikiwa
na Mnyele.
Lakini katika ujumla wake, utumishi wa umma unapasa
‘kutawaliwa’ na utayari wa mtu ‘kujikana’ mwenyewe, kujiondoa katika kuyatafuta
yaliyo ya binafsi na badala yake kujielekeza zaidi kwenye masuala ya
kulitumikia taifa na kuwahudumia watu.
Nadharia hiyo inatoa nguvu ya sababu zinazotajwa kuwa kishawishi
kwa Mnyele kujiuzulu, kwamba anataka kujihusisha na masuala binafsi. Nafsi
inapomtuma mtu kuyafanya yanayokidhi matakwa binafsi, anapaswa kusikilizwa na
kupewa fursa hiyo.
Vinginevyo, kuendelea kuwapo madarakani kimwili huku
fikra zake zikijikita katika kutafuta na kuendeleza masuala binafsi, ndipo
kunapotokea mgongano wa maslahi. Mhusika anabaki kuwa katika mapambano dhidi ya
matamanio ya nafsi yake.
Kwa bahati mbaya, si katika Tanzania bali nchi nyingi
hasa zinazoendelea, baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa wakitumia nyadhifa walizonazo
kama nyenzo ya kuyafikia maslahi binafsi.
Wanajitoa katika kuyafikiri na kuyafanyia kazi yaliyo
yenye manufaa kwa umma, badala yake wanatumia fursa za kuwamo katika utawala
ili kuyafikia mahitaji na matamani yao binafsi.
Hivyo, Mnyele anapojizulu kupitia sababu ya kupata fursa
pana ya kushughulika na masuala binafsi, maana yake rahisi ni kwamba ameuepuka
mgongano wa maslahi. Kwamba angeweza kubaki kulitumikia taifa akiwa Mkuu wa
Wilaya huku nafsi yake ikiwa katika matamanio ya kuyafikia mafanikio binafsi.
Kuyatafuta na kuyafikia mafaniko binafsi si dhambi kwa
mtu, maana kila mwenye nafsi anapaswa kustawisha maisha yake, ya familia,
ndugu, jamaa na taasisi alizo mshirika kama dhehebu la dini anaposali na
kuabudu.
Kwa hiyo Mnyele alipoisikia sauti ikimhitaji kujiweka
kando dhidi ya fursa ya kuwa Kiongozi wa umma aliye mwakilishi wa Rais wa nchi
katika ngazi ya wilaya, anastahili pongezi, ameendeleza kudhihirisha namna
taifa linavyoendeleza misingi ya haki zinazotokana na uhuru wa mtu kufanya
uamuzi usiokinzana na matakwa ya sheria.
Isingekuwa rahisi kwa taifa lenye utawala wa kidikteta
kumuacha Mkuu wa Wilaya anayetumia kigezo cha matakwa binafsi kutoka katika
kuwaongoza watu, atimize nia hiyo pasipo kujali athari kwa uchumi, utawala na uongozi.
Viongozi wa umma wanapaswa kufikiria asili ya nafasi
walizokabidhiwa kama dhamana, iwe kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi,
kuteuliwa ama kuajiriwa. Haifai kwa viongozi wa umma kung’ang’ania madarakani
ama katika uongozi hata pale wanapojitambua kwamba hawafai kulitumikia taifa
kwa mujibu wa dhamana waliyopewa.
Pamoja na taswira hiyo inayolenga uadilifu katika
utumishi wa umma, kutumia uhuru wa kujieleza na kujiweka kando dhidi ya mgongano
wa maslahi, kuna uwezekano Mnyele akawa katika mazingira magumu ya kisiasa.
Atakuwa katika mazingira magumu ikiwa ataendeleza ndoto
za kujiimarisha zaidi kisiasa baada ya ‘kutia nia’ ya kuwania ubunge kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.
Hata hivyo Mnyele alishindwa katika kura za maoni na
hatimaye Sebastian Kapufi akashinda katika kura za maoni na kwa Uchaguzi Mkuu,
hivyo kuwa Mbunge.
Hoja itakayoibuliwa ikiwa Mnyele atahitaji tena kuwania
ubunge, ni pamoja na dhamira iliyomtuma kujiondoa ndani ya mfumo wa kuwatumikia
wananchi. Kwamba kama sababu ya kwenda kufanya shughuli binafsi itakuwa msingi
wa kujiuzulu kwake, ataaminika vipi ikiwa atataka kuwania nafasi kama ubunge?
Pili, kama ameteuliwa na Rais John Magufuli ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, akajizulu kutoka nafasi muhimu katika utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho, je, ataaminika katika nafasi gani nyingine
inayompa fursa ya kuchangia maendeleo yenye kuimarisha imani ya wananchi wengi
kwa chama hicho?
Lakini kwa ujumla wake, Mnyele amejiuzulu nafasi yake kwa
sababu zinazotajwa, hivyo kuwa mfano kwa wengine wakiwamo wasioendana na kasi
ya Rais Magufuli. Kila la heri!
Mashaka Mgeta- 0754691540
0 comments:
Post a Comment