Suleiman Msuya
WAKUU wa mikoa minane nchini wamezungumzia
ukame na ukosefu wa chakula katika maeneo yao.
Wakizungumza na gazeti hili juzi, wakuu
wa mikoa hao walionesha kuvalia njuga hali
hiyo na kuchukua hadhari.
Waliozungumza ni wakuu wa mikoa ya
Pwani, Mwanza, Kilimanjaro, Singida, Iringa, Kigoma, Mtwara na Ruvuma.
Pwani;
Everist Ndikilo alisema mkoa wake umetuma wataalamu
wa ngazi zote kukusanya taarifa za hali ya chakula na kuahidi kuzungumzia suala
hilo hivi karibuni.
“Ni kweli tunaifanyia kazi taarifa hiyo
ya kuwepo njaa kwenye mkoa wangu, nimetuma wataalamu ambao watakuja na taarifa
ambayo itaonesha hali halisi,” alisema.
Mwanza;
John Mongela alisema hana taarifa rasmi ya hali ya
chakula mkoani mwake ila ameagiza ngazi ya wilaya, kata na vijiji kutoa taarifa
na Jumanne ijayo, atakuwa na taarifa sahihi.
Mongela alisema ni kweli zipo taarifa za
njaa ila ni vigumu kubainisha hali halisi ilivyo kabla ya kupata taarifa
sahihi.
Kilimanjaro;
Saidi Sadick alisema baada ya mavuno ya mwaka jana
walipata akiba ya zaidi ya tani 63,000 lakini kutokana na biashara huria upo
uwezekano wa kiasi hicho kupungua.
Alisema wapo wafanyabiashara waliokuwa
wanapitisha mazao kwa njia za magendo wilayani Rombo, hali ambayo inaweza
kuchangia upungufu wa chakula.
“Sisi tunatoa elimu kwa wananchi, ili
kutunza mazao na kama wameishiwa chakula wauze hata mifugo, wanunue kwani hali
ya mvua haitabiriki kwa sasa,” alisema.
Singida;
Dk Rehema Nchimbi alisema mkoa wake ulivuna zaidi
ya tani 762, 202 ambapo mahitaji ni tani 435,125 hivyo kubaki na ziada ya zaidi
ya tani 300,000.
Nchimbi alisema pamoja na mavuno hayo,
wakulima wengi waliuza mazao hayo hali ambayo inaweza kuchangia ukosefu wa
chakula kwa siku za karibuni.
“Tumetuma wataalamu wetu kwenye baadhi
ya wilaya ambazo kimsingi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya chakula kama
Itigi, Manyoni, Mkalama na Iramba hapo tutapata hali halisi ya chakula,”
alisema.
Iringa;
Amina Masenza alisema mkoa wake ulikuwa na akiba
kidogo, hivyo ni dhahiri kuwa upo uwezekano wa changamoto ya chakula kutokea.
Alisema mkoa wake umevamiwa na
wafanyabiashara, hali ambayo inaweza kuchochea upungufu huo, huku akitaka
wananchi kuhifadhi chakula na kulima mazao ya muda mfupi.
Kigoma;
Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga: “Katika
mkoa wa Kigoma hatuna historia ya njaa, kwa sababu ardhi yetu ina rutuba hivyo
siwezi kufikiria kuwa njaa itatokea, kwani mvua zimeanza na wakulima wako mashambani.
Alisema mwaka jana walivuna zaidi ya
tani milioni 1.1 huku mahitaji ya mkoa yakiwa ni zaidi ya tani 500,000 hivyo kuwa
na ziada ya zaidi ya tani 590,000.
Alsema wananchi wake wamekuwa wakiuza
mazao yao mikoa ya jirani ikiwa ni pamoja na kujihusisha na kilimo cha muda
mfupi, hivyo kujihakikishia chakula kila siku.
Mtwara;
Halima Dendegu alisema mkoa wake ulivuna tani zaidi
ya 875,000 ambapo mahitaji kwa mwaka ni zaidi ya tani 460,000 hivyo kuwa na ziada
ya zaidi ya tani 400,000.
Alisema pamoja na mavuno hayo, wamekuwa
wakisisitiza wananchi kulima mazao kama muhogo, ambayo yanahimili ukame na
kuhifadhi fedha za mauzo ya korosho ili ziwasaidie kununua chakula.
Ruvuma;
Dk Binilith Mahenge alisema mkoa wake hauna uhaba
wa chakula na kuwa katika mavuno ya mwaka jana, walipata zaidi ya tani 850,000 ikilinganishwa
na mahitaji ya zaidi ya tani 400,000 kwa mwaka hivyo kuwa na ziada ya tani
400,000.
Alisema kiasi hicho cha zaidi ya tani
800,000 ni kwa mazao ya mahindi pekee ila kwa ujumla wa mazao yote, walivuna
zaidi ya tani milioni 1.7.
Manyara;
Dk Joel Bendera alisema mkoa wake una maeneo ambayo
ukame ulikuwa mkubwa, hali ambayo inaweza kuhatarisha upatikanaji wa chakula.
Bendera alisema mikakati ya mkoa wake ni
kuhamasisha kila mwananchi anatunza chakula alichonacho ili hali ikiwa mbaya zaidi
aweze kukabiliana nayo.
“Hali ya mabadiliko ya tabia nchi
inatishia usalama wa chakula hasa ukizingatia mkoa wa Manyara unategemea Hanang,
Babati na Mbulu, hivyo tunahamasisha kilimo cha muda mfupi,” alisema.
Tabora;
Aggrey Mwanri alisema hali ya chakula mkoani mwake ni
nzuri kiasi na kuwa wanachofanya sasa ni kuhamasisha kilimo cha kisasa.
“Hofu kubwa inatokana na mabadiliko ya
tabianchi ambayo yamekuwa yakitokea kwa kasi kubwa hivyo kinachohitajika ni
wananchi kulima kilimo cha muda mfupi,” alisema.
Jitihada za JAMBOLEO kupata wakuu wa
mikoa mingine zilishindikana kwa baadhi yao simu zao kuita bila kupokewa huku za
wengine zikiwa hazipatikani.
0 comments:
Post a Comment